1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanamgambo wawili wa kike wauwawa Uturuki

Admin.WagnerD3 Machi 2016

Polisi mjini Istanbul Alhamisi (03.02.2016) hii imewauwa wanawake wawili waliokuwa wamejificha ndani ya jengo moja baada ya kuwashambulia polisi kwa risasi na bomu la guruneti.

https://p.dw.com/p/1I6Jj
Polisi wakifunga njia katika kitongoji cha Bayrampasa mjini Istanbul. (03.02,2016)
Polisi wakifunga njia katika kitongoji cha Bayrampasa mjini Istanbul. (03.02,2016)Picha: Reuters/O. Orsal

Katika kitongoji cha Bayrampasa mjini Istanbul kikosi maalum na polisi vililizingira jengo ambapo wanawake hao wawili walijificha na kupelekea majibizano ya risasi yaliodumu kwa saa nzima kabla ya polisi kuwaua wanawake hao.

Shirika la habari la serikali Anadolu bila ya kutaja duru zake limesema wanawake hao wametambuliwa kuwa ni wanachama wa kundi la sera kali za mrengo wa kushoto lililopigwa marufuku linalojulikana kama jeshi la ukombozi la wananchi DHKP-C.

Mkanda wa video wa usalama umewaonyesha wanawake hao wakilifyatulia risasi basi la polisi nje ya kituo cha polisi wa kuzuwiya kufujo katika kitongoji cha Bayrampasa na pia kuvurumisha guruneti kabla ya kuanza kulenga mashambulizi yao dhidi ya kituo hicho cha polisi.Bomu hilo la mkono halikuripuka.

Kufuatia mashambulizi hayo walikimbia kwa kutumia gari na baadae kujificha kwenye jengo moja ilioko masafa mafupi kutoka kituo hicho cha polisi. Kikosi maalum kililizingira jengo hilo kwa haraka na kuanzisha operesheni baada ya wanawake hao kukataa wito wa kusalimu amri na kuanza kuwashambulia polisi.

Mashambulizi ya kundi la DHPK-C

Gavana wa Istanbul Vasip Sahin amesema wanawake hao wote wawili wameuwawa katika operesheni hiyo na polisi wawili wamejeruhiwa mmoja kutokana na vioo vilivyovunjika wakati wa shambulio la basi na mwengine wakati wa kuvamiwa kwa jengo walikojificha wanawake hao.

Hali ilivyokuwa katika kitongoji cha Bayrampasa mjini Istanbul. (03.02,2016)
Hali ilivyokuwa katika kitongoji cha Bayrampasa mjini Istanbul. (03.02,2016)Picha: Reuters/O. Orsal

Miongoni mwa mashambulizi yaliofanywa na kundi hilo la DHPK-C ni mripuko wa kujitowa muhanga katika ubalozi wa Marekani hapo mwaka 2013 ambao umeuwa mlinzi mmoja. Wanamgambo wa kundi hilo pia waliwahi kuufyatulia risasi ubalozi mdogo wa Marekani mjini Istanbul mwaka jana.

Shambulio la leo linakuja wakati Uturuki ikikabiliana na kuibuka kwa matumizi ya nguvu tokea majira ya kiangazi mwaka jana.

Mchakato wa amani ulio lege lege kati ya serikali na chama cha Wafanyakazi cha Kurdistan PKK ulisambaratika mwezi wa Julai mwaka jana na kuufufuwa upya mzozo ambao umeuwa maelfu ya watu nchini Uturuki tokea mwaka 1984.

Kuibuka kwa matumizi ya nguvu

Mwezi uliopita mripuko wa kujitowa muhanga kwa kutumia gari uliolenga mabasi yaliokuwa na wafanyakazi wa kijeshi katika mji mkuu wa Ankara umeuwa takriban watu 29. Kundi la kijeshi ambalo ni tawi la PKK limedai kuhusika na shambulio lakini serikali inasisitiza kwamba huo ulikuwa ni mkono wa kundi la wanamgambo wa Kituruki lilioko Syria kwa kushirikiana na kundi la PKK.

Kituo cha polisi kilichoshambuliwa katika kitongoji cha Bayrampasa mjini Istanbul. (03.02,2016)
Kituo cha polisi kilichoshambuliwa katika kitongoji cha Bayrampasa mjini Istanbul. (03.02,2016)Picha: Reuters/M. Sezer

Takriban watu 145 wameuwawa tokea mwezi wa Julai mwaka jana katika mashambulio matatu tafauti ya miripuko ya mabomu ambayo serikali imelilaumu kundi la Dola la Kiislamu kwa kuhusika.Watalii wa Kijerumani 11 ni miongoni mwa waliouwawa katika kitongoji cha kihistoria cha Sultanahmet mjini Istanbul hapo Januari 21.

Wanajeshi watatu wa Uturuki na wanamgambo 10 wameuwawa hapo jana wakati wa operesheni za usalama katika jimbo la Mardin karibu na mpaka wa Syria.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AP

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman