1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanariadha waanza kuwasili London

16 Julai 2012

Wanariadha wameanza kuwasili katika kijiji cha Olimpiki mjini London huku,hali ikiashiria kuwa mashindano ya mwaka huu ya olimpiki huenda yakagubikwa na mvua za mara kwa mara.

https://p.dw.com/p/15YcQ
China's Sun Yang raises his national flag after winning the gold medal in the men's 1,500m Freestyle event at the FINA Swimming World Championships in Shanghai, China, Sunday, July 31, 2011. (ddp images/AP Photo/Eugene Hoshiko)
Wanariadha watakaopambana katika michuano ya olimpiki mjini LondonPicha: AP

Katika hali ya majira ya joto nchini Uingereza , hali ya hewa haionekani kuwa nzuri sana kuwakaribisha wanariadha hao. Hata hivyo baadhi ya nyumba ambazo wanariadha watakaa kwa muda wa wiki tatu za mashindano ya olimpiki yanayoanza tarehe 27 mwezi huu, tayari zimepakwa rangi za taifa za mataifa hayo yanayoshiriki.

Viwango vya usalama kwa ajili ya mashindano hayo ya olimpiki havijaathirika na kushindwa kwa kampuni iliyopewa jukumu la usalama , kamati ya kimataifa ya olimpiki imesema leo Jumatatu.

Ulinzi waimarishwa

Wiki iliyopita serikali ya Uingereza imesema kuwa itaweka wanajeshi wa ziada 3,500 baada ya kufahamika kuwa kampuni ya ulinzi wa usalama ya G4S haitaweza kupata walinzi 10,400 ambapo kampuni hiyo ilipewa jukumu la kuwapata kutokana na matatizo ya kuwahakiki watu walioomba kazi hiyo.

Usalama umekuwa suala la juu katika orodha ya mambo yanayotia wasi wasi watayarishaji katika michezo hiyo ya mjini London tangu pale vijana wanne wa Kiislamu kuwauwa watu 57 katika shambulio la kujitoa mhanga katika mji huo siku moja baada ya London kuteuliwa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo Julai 2005.

Kiongozi atekwa nyara

Na huko mjini Tripoli nchini Libya taarifa zinasema kuwa rais wa kamati ya olimpiki ya nchi hiyo Nabil al-Alam ametekwa nyara na watu wenye silaha katikati ya mji wa Tripoli na kupelekwa katika maeneo ya siri.

Watu tisa wakijifanya kuwa ni wanajeshi wa jeshi la Libya walimchukua al-Alam kutoka katika gari yake na kumpeleka katika eneo ambalo halijulikani hadi sasa.

Afisa mkuu katika ofisi ya Al-Alam , Arafat Juwan amesema kuwa jeshi na wizara ya mambo ya ndani haina habari juu ya kukamatwa huko.

FIFA yakumbwa tena na kashfa

Wakati huo huo , kamati ya olimpiki ya kimataifa IOC, itajadili kashfa ya rushwa inayowahusisha maafisa wa ngazi ya juu wa shirikisho la kandanda duniani FIFA katika mkutano wake wa bodi ya utendaji mjini London wiki hii, lakini imeondoa uwezekano wa kuweka vikwazi dhidi ya mjumbe wa zamani wa bodi hiyo Joao Havelange.

BERLIN, GERMANY - JUNE 25: Joseph S. Blatter, President of FIFA attends the FIFA Women's World Cup 2011 opening press conference at Olympic stadium on June 25, 2011 in Berlin, Germany. (Photo by Martin Rose/Bongarts/Getty Images)
Rais wa FIFA Sepp BlatterPicha: Getty Images

Mwendesha mashtaka wa Uswisi amesema katika waraka wa kisheria uliotolewa wiki iliyopita kuwa rais wa zamani wa FIFA na mjumbe wa IOC, Havelange na mjumbe wa kamati ya utendaji ya FIFA Ricardo Teixeira walipokea mamilioni kadha ya rushwa katika makubaliano mbali mbali ya kombe la dunia katika miaka ya 1990 kutoka katika shirika la mauazo ya matangazo ya michezo ambalo hivi sasa limevunjika la ISL .

Rais wa sasa wa FIFA Sepp Blatter , ambaye pia ni mjumbe wa IOC , amekana kujua lolote kuhusu kashfa hiyo wakati huo.

Rais wa IOC Jacques Rogge amesema leo kuwa anatarajia kashfa hiyo itajadiliwa katika mkutano huo.

Shirikisho la soka barani Africa CAF itaandika historia mpya katika mwezi August wakati timu tatu kutoka nchi moja zitakapochuana katika michuano ya makundi ya mashindano ya vilabu ya kombe la shirikisho kwa mara ya kwanza. Vilabu vya Al Ahly, Al Hilal na Al Merreikh viko katika kundi A la michuano ya shirikisho la kandanda la Afrika CAF pamoja na Inter Club ya Angola ambayo ilifikia nusu fainali ya mashindano hayo mwaka jana, 2011.

Kupangwa kwa michuano hiyo kuna maana timu hiyo ya jeshi la polisi ya Angola itatembelea nchini Sudan , mwezi August, Septemba na Oktoba.

Katika kundi B ziko timu za Djoliba na Stade Malien zote za Mali, AC Leopards ya Congo, Brazaville na Wydad Casablanca ya Morocco.

Michuano ya Afrika mashariki na kati yanguruma

Michuano ya kuwania ubingwa wa vilabu katika Afrika mashariki na kati imeanza rasmi mjini Dar Es Salaam siku ya Jumamosi wakati timu Dar Young Africans ilipofungua dimba na Atletico ya Burundi, ambapo mabingwa hao watetezi Yanga ilibugia mabao 2-0, wakati APR ya Rwanda iliigaragaza El Salaam ya Djibouti kwa mabao 7-0. Simba nayo ya Tanzania ilikwaa kisiki jana Jumapili baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya URA ya Uganda, ambayo wawakilishi wengine wa Tanzania Azam ya Dar Es Salaam na Mafunzo ya Zanzibar zilitoshana sare ya bao 1-1.

Leo ni mapumziko na kesho michuano hiyo inaanza tena.

Ni Jamhuri Kihwelu Julio akitoa tathmini yake kuhusu pale timu za Tanzania ziliposhindwa kufanya vizuri katika michezo ya mwanzo ya kombe la vilabu vya Afrika mashariki na kati , michuano inayofanyika mjini Dar Es Salaam.

Shirikisho la kandanda nchini Urusi RFU , limemteua kocha raia wa Italia Fabio Capello kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya nchi hiyo na kuamsha vuguvugu la majaaliwa yake baada ya kushindwa kuwika katika fainali za kombe la mataifa ya Ulaya , Euro 2012 iliyofanyika nchini Poland na Ukraine.

epa03094886 England manager Fabio Capello takes his seat in the stands for the English Premier League soccer match between Liverpool and Tottenham at Anfield in Liverpool, Britain, 06 February 2012. EPA/LINDSEY PARNABY DataCo terms and conditions apply http//www.epa.eu/downloads/DataCo-TCs.pdf +++(c) dpa - Bildfunk+++
Kocha mpya wa timu ya taifa ya Urusi Fabio CapelloPicha: picture-alliance/dpa

Rangers yashushwa daraja

Nayo Dundee United itachukua nafasi ya Glasgow Rangers katika ligi kuu ya Scottland SPL , msimu ujao imetangazwa leo Jumatatu.

Rangers vigogo wa soka nchini Scottland waliondolewa kutoka liigi kuu baada ya mwishoni mwa msimu uliopita kufuatia matatizo makubwa ya kifedha ambayo yameshuhudia klabu hiyo yenye historia ya miaka 140 kufikia kuwekwa katika uangalizi wa kifedha.

Wameshushwa hadi daraja la tatu Ijumaa wiki iliyopita , ambayo ni sawa na daraja la nne katika ligi ya soka ya Scottland.

New Castle ya Uingereza inajaribu kupata saini ya mshambuliaji wa Liverpool Andy Carroll na kumrejesha St James Park . Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23 wa Uingereza aliondoka kutoka timu hiyo na kujiunga na mahasimu wao katika ligi kuu ya Uingereza Liverpool kwa kitita cha pauni milioni 35 Januari mwaka jana.

Mwandishi : Sekione Kitojo

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman