Wanasiasa nchini Ujerumani wajadiliana sera ya uhamiaji
3 Septemba 2024Waziri wa Mambo ya Ndani katika jimbo la Hesse, magharibi mwa Ujerumani Roman Poseck amenukuliwa akisema kuna umuhimu wa kuifanyia mageuzi makubwa sera ya uhamiaji. Poseck, kutoka chama cha Christian Democratic Union, CDU akaongeza kuwa kwa mtizamo wake anadhani matokeo yanatakiwa kuonekana ndani ya kipindi kifupi.
Katibu Mkuu wa chama cha FDP, kinachopendelea wafanyabiashara, Bijan Djir-Sarai kwa upande wake aliliambia shirika la habari la DPA kwamba ikiwa sera ya uhamiaji haitabadilika, kuna mashaka ya demokrasia kuvurugwa kwa kiasi kikubwa.
Kansela Olaf Scholz baada ya kisa hicho cha Solingen pia alizungumzia umuhimu wa kuzibadilisha sera za uhamiaji, na vizuizi vipya kwa waomba hifadhi lakini pia mamlaka makubwa zaidi ya polisi katika kushughulikia vitisho vya kiusalama. Chini ya mapendekezo hayo, waomba hifadhi waliojiandikisha kwenye nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Ulaya hawatatakiwa kupata stahiki nchini Ujerumani.
Hata hivyo, Kansela Scholz hii leo haudhurii mkutano huo ambao badala yake unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Nancy Faeser kwa niaba ya serikali ya shirikisho. Waziri wa Sheria Marco Buschmann pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje Annalena Baerbock pia wanahudhuria.
Upinzani wanataka wahamiaji haramu kurejeshwa wakifika mipakani
Maafisa wa ngazi za juu wanaowakilisha majimbo yote 16 ya Ujerumani pia wanahudhuria pamoja na wabunge wawili waandamizi kutoka kundi la upinzani la vyama ndugu vya CDU/CSU Thorsten Frei na Andrea Lindholz ni miongoni mwa waliohudhuria pia.
Mshitakiwa wa kisa hicho cha Agosti 23, anahisiwa kuwa ni mtu mwenye misimamo mikali kutoka nchini Syria na amekuwa akipinga kurudishwa nyumbani hivi sasa anazuiliwa kizuizini kwa mashtaka ya mauaji, lakini pia akihisiwa kuwa ni mfuasi wa kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.
Shambulizi la Solingen lilitokea baada ya kisa kingine cha afisa wa polisi aliyeuliwa na mhamiaji kutoka Afghanistan, katika mji wa Mannheim mapema mwezi Juni.
Soma pia:Scholz atembelea Solingen kulikofanyika shambulio la kisu
Kiongozi mkuu wa upinazni nchini Ujerumani Friedrich Merz wa CDU alinukuliwa akisema kabla ya mazungumzo haya kwamba uhamiaji usiodhibitiwa ndilo hasa suala la msingi linalotakiwa kushughulikiwa. Akasema "ikiwa muungano wa serikali unataka kusikia suluhisho kutoka kwetu, basi ajenda ya kwanza itakuwa ni kupunguza wahamiaji". Ametaka wahamiaji wanaoingia kinyume cha sheria kurejeshwa makwao mara moja wakiwa hukohuko mpakani.
Akasema hakuna namna nyingine ya kumaliza tatizo, ispokuwa kwa "kuwarejesha tu".
Sikiliz a pia: