1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaume watatu wafunguliwa mashtaka ya ugaidi Ubelgiji

26 Machi 2016

Waendesha mashtaka nchini Ubelgiji wamewafungulia mashtaka wanaume watatu kwa makosa ya ugaidi akiwemo mtuhumiwa ambaye vyombo vya habari vimesema alionekana kwenye kamera ya usalama ikatika uwanja wa ndege wa Brussels´.

https://p.dw.com/p/1IKJN
Wanajeshi wa Ubelgiji kwenye barabara ya kuelekea uwanja wa ndege mjini Brussels
Wanajeshi wa Ubelgiji kwenye barabara ya kuelekea uwanja wa ndege mjini BrusselsPicha: Reuters/C. Platiau

Waendesha mashtaka wamemtaja mtuhumiwa huyo wa watatu kwa jina la Feycal C. wakati vyombo vya habari vimemtambulisha kwa jina la Faycal Cheffou na kusema kwamba alikuwa ndie mwanaume aliyevaa kofia na koti jeupe katika picha ya uwanja wa ndege ya Ijumanne iliopita ambayo imewaonyesha wanaume watatu wakisukuma vitoroli vya mizigo.

Waendesha mashtaka wamesema amefunguliwa mashtaka kwa kujihusisha na harakati za kundi la kigaidi na kutenda pamoja na kujaribu kufanya mauaji ya kigaidi.Nyumba yake ilipekuliwa lakini hakuna silaha wala viripuzi vilivyopatikana.

Wanaume wengine wawili Aboubakar A. na Rabah N. pia walifunguliwa mashtaka ya kujishughulisha na harakati za kigaidi na kuwa wanachama wa kundi la kigaidi.Rabah N . alikuwa akitafutwa kuhusiana na msako uliofanyika nchini Ufaransa wiki hii ambapo serikali imesema imegunduwa njama ya kufanya mashambulizi.

Fadhaa barani Ulaya

Jumla ya watu 31 wameuwawa wakiwemo washambuliaji watatu na wengine 300 kujeruhiwa katika mashambulizi yaliofanyika katika uwanja wa ndege na kituo cha reli cha chini ya ardhi mjini Brussels ambapo kundi la Dola la Kislamu limedai kuhusika.

Wanajeshi wa Ubelgiji katika kituo kikuu cha treni mjini Brussels.
Wanajeshi wa Ubelgiji katika kituo kikuu cha treni mjini Brussels.Picha: picture-alliance/dpa/F. Gambarini

Mashambulizi hayo ya Brussels makao makuu ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO na Umoja wa Ulaya yamekuja miezi minne baada ya wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu kuuwa watu 130 mjini Paris na kuzusha fadhaa barani Ulaya na duniani kwa jumla.

Kutokana na kuongezeka kwa dalili kwamba mashambulizi hayo ya Brussels na Paris yametekelezwa na wanachama wa kundi moja polisi barani Ulaya wamewakamata watu tisa wakati wa misako nchini Ubelgiji na wawili nchini Ujerumani kabla ya mwisho wa juma.

Ni mtu hatari

Cheffou ambaye vyombo vya habari vinasema ni mwandishi wa habari wa kujitegemea alitambuliwa na dereva wa taxi ambaye aliwapakia washambuliaji kuwapeleka uwanja wa ndege hapo tarehe 22 Machi.

Mtuhumiwa wa ugaidi aliyetambiulika kwa jina la Faycal. C
Mtuhumiwa wa ugaidi aliyetambiulika kwa jina la Faycal. CPicha: picture-alliance/dpa/Federal Police

Awali polisi ilisema yumkini akawa ndie mtu wa tatu aliyeonekana na kamera za usalama uwanja wa ndege.

Meya wa mji wa Brussels Yvan Mayeur ameliambia gazeti la Le Soir kwamba mwandishi huyo anayejitangaza kuwa wa kujitegemea amekamtwa katika bustani mara kadhaa akiwashawishi waomba hifadhi waliopiga kambi hapo kujiunga na itikadi kali.Amesema ni mtu hatari na alikuwa amepigwa marufuku kwenda kwenye bustani hiyo.

Operesheni ya polisi yaendelea

Dalili ya operesheni kubwa ya polisi imeendelea kuwepo Jumamosi katika kitongoji cha Schaerbeek mjini Brussels ambapo mwanaume mmoja alipigwa risasi katika kituo cha reli.

Polisi wa Ubeigiji katika operesheni ya kupambana na ugaidi Brussels.
Polisi wa Ubeigiji katika operesheni ya kupambana na ugaidi Brussels.Picha: Reuters/V. Kessler

Mwanaume huyo ambaye alikuwa amekiti na msichana mdogo na aliyekuwa ameshikilia mkoba aliamuriwa na polisi kuuweka mkoba huo mbali naye na baada ya kufanya hivyo polisi ilimpiga risasi mara mbili.

Serikali ya Ubelgiji imewataka wananchi kutojiunga na "Maandamano didi ya hofu " yaliopangwa kufanyika Jumapili kutokana na wasi wasi wa usalama na kupendekeza maandamano hayo yaahirishwe kwa wiki kadhaa.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri : Sudi Mnette