Wanawake Afghanistan waandamana mjini Kabul
29 Novemba 2022Wanawake nchini Afghanistan waliandamana kwa muda mfupi mjini Kabul wakitaka haki zao zitambuliwe katika mkesha wa Siku ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa ya kutokomesha ukatili dhidi ya wanawake.
Wanawake wa Afghanistan wamebanwa nje ya maisha ya umma tangu kurejea madarakani kwa kundi la Taliban Agosti mwaka jana, lakini vikundi vidogo vimefanya maandamano ambayo kwa kawaida huzimwa haraka, wakati mwingine kwa vurugu.
Wanamgambo wa Taliban walifuatilia kwa karibu maandamano hayo, huku magari yenye nembo ya huduma za kijasusi yakizunguka katika eneo hilo.
Wanawake wengi wafanyikazi wa serikali wamepoteza kazi zao au wanalipwa pesa kidogo kukaa nyumbani tangu Taliban kurejea madarakani na wamezuiwa kusafiri bila ndugu wa kiume, na lazima wajifunike kwa vazi la burqa au hijabu wanapokuwa nje ya nyumba.
Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake kwa kawaida huadhimishwa duniani kote tarehe 25 Novemba.