1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Wanawake Kongo wamtaka Rais Tshisekedi kukomesha ukatili

7 Machi 2024

Wanawake wanaokimbia mapigano kati ya jeshi na waasi wa M23 wamemlalamikia Rais Félix Tshisekedi wakimtaka kukomesha ukatili na ubakaji unaofanywa na makundi yenye silaha nchini Kongo

https://p.dw.com/p/4dGJY
Mama na mwanawe katika kambi ya wakimbizi
Kina mama na watoto ndio wanaoathirika pakubwa katika machafuko ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Edith Kimani/DW

Wakati vita vikiendelea kusambaa katika baadhi ya maeneo mkoani Kivu Kaskazini huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wanawake wanaokimbia mapigano kati ya jeshi na waasi wa M23 wamemlalamikia Rais Félix Tshisekedi wakimtaka kukomesha vitendo vya ubakaji na ukatili wanaofanyiwa na makundi yenye silaha. 

Katika visa vingi, walionusurika wanasema walishambuliwa na watu wenye silaha waliowadhalilisha kingono, kama anavyoeleza mama huyu mkimbizi anayeishi sasa ndani ya kambi moja nje kidogo na mji wa Goma: "Kila mwanamke anayo haki ya kuishi. Mwenyewe ujiulize jinsi gani unaweza kubakwa wakati mume wako amewekewa silaha kichwani tena ukiwa pembezoni na mwanao. Sasa rais unayo mawazo gani kuhusu sisi. Tazama watoto wetu hawaendi shule tena. Tunahitaji kurudi nyumbani kwetu Masisi." Alisema mama mmoja

Wanawake waandamana kutaka vita kukomeshwa DRC

Kukosa makaazi na mahitaji muhimu pia ni changamoto kubwa kwa wanawake hao wanaohangaishwa na vita na ambao wanalazimika kulala kandoni mwa barabara mjini Goma. Vumilia Esperance akiwa pamoja na watoto wake sita, wanatumia majani ya migomba kama godoro la kulalia:

"Wanawake tunalala uwanjani, ndani ya nyumba za hema ambamo mawe yamejaa kwa wingi. Ona jinsi vyandarua vinatumiwa hapa kama mabati. Ni mateso mno. Kama mama wa watoto sita lakini unalala vibaya ndani ya nyumba yenye kujengwa na chandarua. Kweli tunasumbuka."

Wanawake hao waliongunana na wenzaao kutoka mashirika ya kutetea haki za wanawake, walisema wana hofu kutokana na kuenea kwa machafuko, ambayo ni sababu ya kuongezeka kwa visa vya ukatili wa kijinsia dhidi yao. PASY MUBALAMA ni kutoka shirika la wanawake liitwalo Tujitetee hapa Kivu Kaskazini: "Sisi kama vile wanawake tumechoshwa na vita. Ni vizuri sasa suluhu ipatikane. Ukimya huu wa jumuiya ya kimataifa dhidi ya visa vya ujeuri hapa nchini Kongo mwenyewe sielewi kabisa."

Makundi mengi ya waasi yanaendesha harakati zao Kongo
Machafuko ya Mashariki ya Kongo yanasababisha watu wengi kuyakimbia makazi yao Picha: Moses Sawasawa/AP/picture alliance

Shirika la Tujitetee pamoja na idara ya maswala ya kijinsia ya Kivu Kaskazini zinakadiria kuwa baina ya Januari mwaka jana na sasa zaidi ya visa 25,000 vya ubakaji vimeripotiwa kutokana na vita vinavyosambaa katika baadhi ya maeneo ya mkoa huu wa Kivu Kaskazini.

Wakati hayo yakiendelea, waasi wa M23 walifaulu kuudhibiti miji ya Nyanzale na Kibirizi wakikaribia sasa kiwanda muhimu cha kuzalisha madini cha SOMIKIVU wilayani Rutshuru karibu kilomita 100 kutoka mji mkuu wa mkoa huu, Goma.

Taarifa zinasema kuwa watu wanaoathirika kwa asilimia kubwa na vita hivyo ni watoto na wanawake wanaohangaika kwa kukimbia mapigano hayo baina ya jeshi la serikali na waasi wa M23.