1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake na Demokrasia nchini Nigeria

16 Aprili 2007

Je wanawake nchini Nigeria wamefaidika vipi na demokrasia katika kipindi cha miaka minane.

https://p.dw.com/p/CHGD
Rais Olusegun Obasanjo wa Nigeria
Rais Olusegun Obasanjo wa NigeriaPicha: dpa

Wanaume ndio wanapaswa kufanya maamuzi yote na wanawake mahala pao ni jikoni wakati wao wanatayarisha chakula basi wanaume nao wanajishuhgulisha na maswala ya siasa.

Huo ndio msemo aliopenda kuutumia bibi Dorothy Ukel Nyone akikumbushia masaibu yaliyomkuta kila alipopata fursa ya kuwaeleza wanaume juu ya nia yake ya kutaka kugombea kiti katika uchaguzi wa uwaskilishi wa majimbo nchini Nigeria uliofanyika jumamosi iliyopita.

Bi Nyone aliyetaka kugombea kiti cha uwakilishi katika eneo la Gokana, kusini mashariki mwa jimbo la Rivers kwa tikiti ya chama tawala cha People’s Demokratik alikuwa na ujasiri mkubwa.

Anasema alitengeneza manifesto yake na kuendelea na kutafuta wafuasi hasa zaidi miongoni mwa wanawake na kwa kufanya hivyo alipata moyo wa kujiamini kuwa atashinda kwanza katika uchaguzi wa mashinani wa chama chake lakini bi Nyone ilimbidi ameze kidonge kichungu, kwani siku ilipowadia ya kuwachaguwa wagombea watakao kiwakilisha chama ndio siku aliyojifunza kwa hakika siasa za Nigeria.

Anasema baadhi ya wagombea walifika kituoni pamoja na makundi ya majambazi na mara ghasia zikazuka kabla ya hata uchaguzi wenyewe kuanza.

Kwa hofu watu walikimbia huku na huko pamoja na yeye na kituoni hapo kukabakia wanaume waliokuwa tayari kuyakabili machafuko hayo na hapo walipata nafasi ya kuchaguwa wawakilishi waliowataka wao.

Mfano huo wa bibi Nyone sio wa pekee bali wanawake nchini Nigeria wanakabiliwa na panda shuka nyingi wanapojitolea kuwapinga wanaume.

Princewill Akpakpan wa shirika la kutetea haki za raia mjini Lagos ameeleza hayo alipozungumza na shirika la habari la IPS.

Tangu Nigeria ilipopata uhuru wake kutoka kwa Waingereza mwaka 1960 hakuna mwanamke aliyewahi kuchaguliwa kuwa gavana wa jimbo hata mara moja usambe kuwa na tamaa ya kuwa na rais mwanamke katika taifa hilo ya Afrika ya Magharibi.

Akpakpan anasema siasa za Nigeria zinategemea yule mwenye nguvu ndie apatae na kwa ajili hiyo wanaume wana uwezo zaidi wa kutumia nguvu kuliko wanawake.

Tatizo jingine linalo wakabili wagombea wanawake ni uwezo wa kifedha kwani wanaume kwa upande huo wamewazidi wanawake kwa hivyo inakuwa rahisi kwao kugharamia shughuli za uchaguzi.

Shirika la maendeleo ya wanawake la Kebetkache ni miongoni mwa makundi yanayojihusisha na harakati za kupigania uwakilishi zaidi wa wanawake katika siasa za Nigeria.

Shirka hilo lina mipango ya kuwasaidia wanawake wanaotaka kuwania viti kuanzia katika uchaguzi wa majimbo ulio malizika hadi ule wa kugombea wa bunge na kiti cha rais unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki.

Bibi Dorothy Ukel Nyone anaamini kwamba vurugu ndio chanzo kikubwa kinachowazuia wanasiasa wanawake kushiriki kikamilifu katika maswala yanayoambatana na siasa na nchi yake Nigeria ina jukumu kubwa la kukiruka kiunzi hicho kipya miaka minane tangu nchi hiyo kuwa chini ya utawala wa kiraia baada ya miaka 16 ya utawala wa kidikteta wa kijeshi.