Biashara ndogondogo zinachangia 40% ya pato la ndani Afrika
7 Desemba 2023Kongamano hilo linafanyika huku ikielezwa kuwa wanawake wanakabiliwa na changamoto lukuki ikiwamo ukosefu wa mitaji na mikopo ya kuendesha biashara.
Asilimia 90 ya biashara zote barani Afrika ni biashara ndogondogo na za kati na asilimia 60 kati ya hizo zinamilikiwa na wanawake. Hayo yameelezwa (07.12.2023) katika kongamano la wanawake chini ya eneo huru la biashara Afrika, linalofanyika jijini Dar es Salaam kwa mara ya pili sasa.
Ni katika mkutano huu unaofanyika chini ya wakfu wa mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (Afcta) ndipo wanawake wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wamekutana kujadili changamoto, fursa na mafanikio waliyoyapata katika mazingira ya biashara ndogondogo na za kati.
Wanawake wanakabiliwa na changomoto nyingi kibiashara
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa Kassim alikuwa ndiyo mgeni rasmi katika kongamano hilo na akaorodhosha changamoto kuu zinazowakabili wafanyabiashara wanawake ikiwamo ukosefu wa mikopo na mitaji yenye masharti nafuu, ukosefu wa taarifa sahihi na vikwazo katika biashara za mipakani.
Pamoja na changamoto hizo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema''Tunaweza kulitumia Eneo la Biashara Afrika, ili kumuwezesha mwanamke, kufanya biashara Afrika. Hii ni pamoja na ustawi wa nchi na maendeleo ya wanawake kwa kasi. Endapo fursa hizi zitatumika basi italeta maendeleo.''
Biashara ndogondogo zinachangia asilimia 40 za pato la ndani Afrika
Kongamano hilo lililowajumuisha wafanyabiashara wanawake kutoka nchi zaidi ya 50 Afrika, viongozi wa ngazi za juu za serikali, mawaziri na makatibu wakuu kutoka nchi hizo, limejadili pia rasimu ya itifaki ya wanawake na vijana katika biashara inayotarajiwa kuanza kutumika Februari 2024.
Washiriki katika kongamano hilo walielezwa kuwa, biashara ndogondogo ndizo zinazochangia asilimia 40 ya pato la taifa katika nchi za Afrika, lakini ndizo zinazokabiliwa na changamoto lukuki.
Himzo la kuondolewa vikwazo vya kibiashara
Katibu Mkuu wa Afcta, Wankele Mene kutoka Afrika Kusini, akatoa wito kuwa ni muhimu kuchukua hatua muhimu kwa kuondoa vikwazo vya kibiashara vinavyowakabili wanawake na vijana Afrika. zaidi aliongeza kwa kusema ''Mkutano huu unatoa fursa za kuchukua hatua, muhimu"
Waziri wa Viwanda na Biashara Tanzania, Dk Ashatu Kijaji amesema mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi, uliofanyika Desemba mwaka jana, ulielekeza nchi za Afrika kuandaa itifaki mahsusi kwa ajili ya wananake na vijana katika biashara na tayari Tanzania imeshaandaa rasimu.
Kongamano hili limeenda sambamba na maonyesho ya wajasiriamali wanawake barani Afrika, ikiwamo Senegal, Morocco, Zambia na Burundi wakionyesha bidhaa na kampuni zao za kibiashara.
Wakati kongamano hili likiingia katika siku yake ya pili hii leo nchini hapa, ripoti iliyochapishwa na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) na Sekretarieti ya AfCFTA, mwaka 2020 imeonyesha kuwa, asilimia 90 ya nguvu katika sekta isiyo rasmi ni wanawake ambao kimsingi bado wanakabiliwa na vikwazo lukuki vya kiuchumi. Florence Majani. DW. Dar es Salaam.
Kongamano hili la Wanawake katika Biashara la AfCFTA, ni kongamano la pili kufanyika ambapo Kongamano la Kwanza lilifanyika Septemba mwaka jana.
Chanzo: DW Dar es Salaam