1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake wajawazito wanaweza kutibiwa Saratani

4 Machi 2012

Watafiti wamesisitiza kuendelea kutolewa kwa taarifa za wanawake waliopatikana na ugonjwa wa saratani wakiwa na ujauzito; kwani sasa kuna matumaini chanya.

https://p.dw.com/p/14EfJ
Vitoto vichanga mara tu baada ya kuzaliwa huko Korea Kusini
Vitoto vichanga mara tu baada ya kuzaliwa huko Korea KusiniPicha: AP

Tafiti zinaonesha kuwa wanawake hawa wanaweza kutibiwa kama wagonjwa wengine wa saratani, bila kuwa na uwezekano wa mtoto aliyepo tumboni kuathirika na tiba hizo.

Mwanamke mmoja mjamzito kati ya 1,000 wanajikuta na tatizo hilo, lakini madaktari wanahisi idadi hiyo itaongezeka kwani athari ya kupata saratani inaenda sambamba na umri ,na wanawake wengi siku hizi huchelewa kupata watoto.

Kwa miaka mingi, madaktari wamekuwa na wakati mgumu kuamua kumtibu mjamzito mwenye saratani au kumwacha ,kwa kuhofia kukiathiri kiumbe ambacho hakijazaliwa, kutokana na tiba ya mionzi na dawa za ugonjwa huo ambazo zina sumu.

Majarida ya Lancet na Lancet Oncology yamechapisha ripoti hiyo mpya na kuonesha matokeo ya utafiti uliofanywa kwa watoto 70 wa barani Ulaya ambao mama zao walipatiwa tiba ya mionzi (chemotherapy) wakiwa tumboni na wakagundulika kukuwa kama watoto wengine, baada ya kuchunguzwa mioyo yao, ukuaji wao wa ubongo na afya yao kwa ujumla.

Watoto hao walifanyiwa uchunguzi wakati wa kuzaliwa, wakiwa na umri wa miezi 18 na kila baada ya miaka michache mpaka walipofikia umri wa miaka 18.

Mjamzito mwenye saratani ya titi akijifanyia uchunguzi
Mjamzito mwenye saratani ya titi akijifanyia uchunguziPicha: Fotolia/Forgiss

Watafiti hao kutoka Ubelgiji wamegundua na kuthibitisha kwamba tiba ya kemikali baada ya mimba kufikia miezi mitatu inawezekana na tiba ya mionzi inaweza kufanyika katika kipindi cha miezi sita ya ujauzito, wakati ambapo kiumbe tumboni ni kichanga mno kiasi cha kuweza kufunikwa na blanketi, kuzuia mionzi kupenya.

Aidha utafiti huo umeonesha kutoa mimba kwa mwanamke mjamzito anayeugua saratani hakumuepushi na kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.

Utafiti mwingine uliofanywa na wanasayansi wa Ufaransa na Marekani unawashauri madaktari kulenga kuokoa maisha ya mtoto aliyepo tumboni iwapo mama mjamzito anaugua saratani ya kizazi, iwapo inawezekana.

Dokta Frederic Amant wa Taasisi ya Saratani ya Leuven nchini Ubelgiji, mmoja wa watafiti hao walionukuliwa na Jarida la Lancet anasema madaktari wengi huhofia kumpa mjamzito mwenye saratani tibakemikali na wengi ni wepesi kutoa mimba za mama hao.

Dokta Amant anasema kumtibu mjamzito huyu mwenye saratani hakuna tofauti yoyote na kumtibu mgonjwa mwingine ambaye si mjamzito.

Kwa upande wake, Dokta Richard Theriault, Profesa katika Kituo cha Saratani cha MD Anderson cha mjini Texas, Marekani anasema matokeo haya mapya ya utafiti yatabadilisha namna ya madaktari wanavyowatibu wajawazito waliothibitika kuwa na saratani.

Dokta Richard ambaye anashughulika na mpango wa kuwatibu wajawazito wenye saratani nchini Marekani anasema kuua watoto wasio na hatia ambao bado hawajazaliwa si muhimu wakati wote. Anasema ni mimba chache kituoni hapo ambazo hutolewa kwa sababu ya wajawazito husika kuugua saratani.

Hapa ndipo wote tulitoka
Hapa ndipo wote tulitokaPicha: Getty Images

Caroline Swain aliyegundulika na saratani ya titi wakati akiwa na ujauzito wa mtoto wake wa pili wa kiume, anasema alipatwa na hofu kubwa baada ya kupata majibu na akadhania kuwa atakufa bila ya mwanae kumuona.

Mkazi huyo wa London, Uingereza mwenye umri wa miaka 45 alikatwa titi lake moja na tezi nyingi kifuani na akasubiri mpaka mimba ilipofika umri wa majuma 12 ndipo alipoanza kupatiwa tiba kemikali.

Luke ambaye ana umri wa miaka tisa sasa, alizaliwa na kilogram 3.35, uzito ambao ni mwepesi kidogo na wa kaka yake Max lakini amekuwa kama mtoto mwingine yeyote, duniani.

Mwandishi: Pendo Paul

Mhariri: Sekione Kitojo