1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Wangari Maathai: Mwanaharakati asiye ogopa

Yusra Buwayhid
3 Machi 2020

Uamuzi wa kupewa Wangari Maathai Tuzo ya Amani ya Nobeli ulishangaza wengi mwaka 2004. Lakini pia ulitilia msisitizo mchango wake kupitia Vuguvugu la Ukanda wa Kijani katika kujenga jamii yenye Amani na iliyo endelevu.

https://p.dw.com/p/3YnnS
DW African Roots | Wangari Maathai

Wangari Maathai: Mwanaharakati asiye ogopa

Yalikuwaje maisha ya awali ya Wangari Maathai?

Wangari Muta Maathai alizaliwa mnamo mwaka 1940 kijiji cha Tetu kwenye nyanda za juu za Kenya, kilomita 160 (maili 99) kutoka mji mkuu wa Naironi nchini Kenya. Alikuwa ni miongoni mwa vijana wa Kiafrika 800 waliopelekwa kusoma nchini Marekani kupitia programu ya masomo ya Kennedy Airlift katika miaka ya 1960.

Ni yepi mafanikio ya kimasomo ya Wangari Maathai?

Alisomea sayansi ya kibaolojia nchini Marekani, alipohamasishwa na Vuguvugu la Harakati za Haki za Raia. Alirudi nchini Kenya na baadae kuelekea Ujerumani kwa masomo ya ziada. Alikuwa mwanamke wa kwanza kutoka Afrika Mashariki na Afrika ya Kati kupata shahada ya udaktari. Na baadae akawa mwanamke wa kwanza Afrika Mashariki na ya Kati kuwa profesa mshiriki. Mwaka 1976 Wangari Maathai alikuwa mwenyekiti wa Idara ya Anatomia ya Mifugo katika Chuo Kikuu cha Nairobi, alikochukua nafasi kama profesa mshirika mwaka uliofuata.

DW African Roots | Wangari Maathai
DW Asili ya Afrika| Wangari Maathai

Vuguvugu la Ukanda wa Kijani la Wangari Maathai lilianzaje?

Maathai alianzisha wazo la kuziwezesha jamii kujisimamia katika kupandisha miti. Wazo hilo alilipanua kwa kuanzisha jumuiya aliyolipa jina la Vuguvugu la Ukanda wa Kijani (GBM). Vuguvugu hilo lilianzishwa mnamo 1977, chini ya usaidizi wa Kamati ya Taifa ya Wanawake wa Kenya (NCWK). Hatua hiyo ilikuwa ni njia ya kupambana na mahitaji ya nishati na maji ya wanawake wa vijijini nchini Kenya. Kadri miaka ilivyosonga mbele, jumuiya ya Maathai ya GBM ilifanikiwa kupanda miti milioni 51 nchini Kenya. Vuguvugu hilo linalofanya kazi katika ngazi ya vitongoji, kitaifa na kimataifa, linalenga kujenga uwezo wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuwawezesha wanawake.

Vipi Wangari Maathai alipigania haki za binadamu?

Maathai alijulikana kwa harakati zake za kupinga suala la upokonyaji wa ardhi pamoja na kupigania uhifadhi wa maeneo ya maji na miti nchini Kenya. Mnamo mwaka  1989, wakati Kenya ikiwa bado chini ya mfumo wa kisiasa wa chama kimoja kilichokuwa kikiongozwa na Rais Daniel Toroitich arap Moi, Maathai alianzisha kampeni dhidi ya ujenzi wa jengo la horofa 60 la gazeti la Kenya Times katika Bustani ya Uhuru - hekta 13 (mita za mraba 130, 000) karibu na eneo kuu la biashara mjini Nairobi.

Muongo mmoja baadae, aliongoza kundi la raia waliokuwa na wasiwasi na wahuni waliotumwa na watu waliokuwa wakitaka kunyakua ardhi na kujenga ndani ya Msitu wa Karura - msitu wa mijini uliyotangazwa katika gazeti la serikali mnamo mwaka 1932 ulioko katikati mji mkuu. Awali ulikuwa na kipimo cha hekta 1,041, lakini kutokana na ujenzi baade ulipungua hadi hekta 564 kulingana na ripoti ya mwaka 2005 inayohusu ugawaji haramu wa ardhi nchini humo.

Wangari Maathai: Mwanaharakati asiye ogopa

Wangari Maathai pia alikuwa anajihusisha sana na harakati za kuanzisha mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi nchini Kenya. Mnamo mwaka 1992, mwaka wa kwanza wa uchaguzi wa vyama vingi, Maathai aliongoza maandamano kwenye Bustani ya Uhuru mjini Nairobi ya kundi la akina mama waliokuwa katika mgomo wa njaa. Wanawake hao walikuwa pamoja na kundi lengine la wanaharakati wa kisiasa linalojulikana kama (RPP) linalodai kuachiliwa huru kwa wafungwa wa kisiasa. Akina mama hao walikuwa wakidai kuachiliwa kwa watoto wao waliofungwa gerezani bila kusikilizwa kesi zao kwa madai yaliyochochewa kisiasa. Wanawake hao walivua nguo zote polisi walijaribu kuyatawanya maadamano hayo. Walisimama kidete kwa muda wa miezi 11 na baada ya hapo serikali iliamua kuwasikiliza na kuwaachilia huru wafungwa hao. Sehemu ya Bustani ya Uhuru baadae ilipewa jina la Kona ya Uhuru kuyakumbuka maandamano hayo.

Baada ya kuanzishwa mfumo wa kisiasa wa vyama vingi, vuguvugu la Ukanda wa Kijani liloongozwa na Maathai ilizielimisha jamii kuhusu utawala bora, jinsi ya kudumisha amani pamoja na kuhifadhi mazingira.

Wangari Maathai aliheshimiwa vipi kwa kazi yake?

Kwa mchango wake huo, Wangari Maathai alipata tunzo kadhaa, miongoni mwao ni Tuzo ya Maisha ya Haki, Tuzo ya Mazingira ya Goldman, Tuzo ya Indira Ghandi  na tuzo kubwa zaidi ya Ufaransa ya Legion of Honor. Mnamo mwaka 2005, alichaguliwa kuwa Balozi wa Mfumo wa Ikolojia wa Msitu wa Bonde la Kongo

Na mwaka 2004 Norway ilimpa Tuzo ya Amani ya Nobeli kwa mchango wake katika maendeleo endelevu, demokrasia, na amani nchini Kenya na bara zima la Afrika.

DW African Roots | Wangari Maathai
DW Asili ya Afrika| Wangari Maathai

Nukuu maarufu za Wangari Maathai!

"Kizazi kinachoharibu mazingira sio kizazi kinachokuja kuathirika. Na hilo ndiyo tatizo."

"Haki za binadamau sio za kuchezewa. Hizi ni haki zinazopiganiwa na baadae kulindwa."

"Leo tunakabiliwa na changamoto ambayo inahitaji mabadiliko katika fikra zetu, ili binadamu waache kutishia mfumo unaosaidia maisha. Huu ni wito wa kuisaidia  Dunia kuponya majeraha yake na, kwa mchakato huo, kuponya majeraha yetu wenyewe - kwa kweli huku ni kuukumbatia uumbaji wote katika utofauti wake, uzuri na majaabu yake. Kutambua kuwa maendeleo endelevu, demokrasia na amani haviwezi kugawanywa ni wazo ambalo wakati wake umefika."

"Mimi ninafahamu sana kwamba huweza kufanikisha kitu peke yako. Ni kazi ya timu nzima. Unapofanya peke yako unajiweka katika hatari kwamba utakapokuwa hupo tena hamna mtu mwengine yeyote atakaekuwa na uwezo wa kuifanya kazi hiyo.

Wangari Maathai atakumbukwaje?

Wangari Maathai alifariki dunia kutokana na saratani ya uzazi mnamo Septemba 25, 2011 akiwa na umri wa miaka 71.

Mwaka 2012, Umoja wa Afrika walitangaza Machi 3, kuwa ni Siku ya Wangari Maathai. Siku hiyo inaadhimishwa sambamba na Siku ya Mazingira Afrika.

Mwaka 2016, Serikali ya Kaunti ya Nairobi imeibadilisha jina la Barabara ya Forest na kuiita Barabara ya Profesa Wangari Maathai.

Taasisi ya Wangari Maathai ya Mafunzo ya Amani na Mazingira (WMI) katika Chuo Kikuu cha Nairobi ilianzishwa ili kuheshimu, kutambua, kusherehekea, kuendeleza, maadili na kazi za Profesa Wangari Maathai.

Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na Taasisi ya Gerda Henkel.