1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina wa umri wote waruhusiwa kuswali Al-Aqsa

14 Novemba 2014

Israel imetangaza kuwaruhusu Wapalestina wa umri wote kuingia na kuswali kwenye msikiti unaozozaniwa wa Al-Aqsa, kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kwenye mazungumzo ya Jordan, Israel, na Marekani.

https://p.dw.com/p/1Dmpb
Msikiti wa Al-Aqsa
Msikiti wa Al-AqsaPicha: AFP/Getty Images/T. Coex

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, ambaye amekuwa kwenye jitihada za kusaka makubaliano ya amani ndani ya kipindi tete cha mzozo wa kisiasa uliogeuka wa kidini, amesema hatua kadhaa zimefikiwa katika mkutano baina yake na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu pamoja na Mfalme Abdullah wa Jordan, ambao umezungumzia kuhusu kuweka mazingira yatakayosaidia kupunguza mvutano katika eneo la msikiti wa Al-Aqsa.

Kerry amesema wamekubaliana kupunguza ghasia zinazoendelea kwa sasa na kwamba pande zote zimeahidi kuchukua hatua za kurejesha hali ya utulivu, kwa lengo la kuepusha machafuko yasiyambae zaidi hadi kufika katika hatua ya kushindwa kudhibitiwa. Hata hivyo, Kerry hakueleza hatua hizo ambazo zitachukuliwa, ingawa amesema mkutano huo pia unaweza kusaidia katika kuyafufua mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina.

Kabla ya mkutano huo uliowajumuisha viongozi hao watatu, Kerry alikutana na Kiongozi wa Palestina, Mahmoud Abbas kwa wakati tofauti hapo jana, na pia alikutana na Mfalme Abdullah siku ya Jumatano. Katika mazungumzo yake na Kerry, Mfalme Abdullah alitaka kumalizika kwa kile alichokiita ''vitendo vya uchokozi vya mara kwa mara vya Israel'', katika eneo takatifu.

Aidha, Kerry alielezea yale aliyothibitishiwa na Abbas katika kukabiliana na mzozo huo. '' Rais Abbas ameelezea tena azma yake ya kutaka kutumia njia za amani ili kumaliza ghasia na ametangaza wazi kufanya kila linalowezekana kurejesha utulivu na kuzuia uchochezi wa vurugu na kujaribu kuibadilisha hali iliyopo,'' alisema Kerry.

John Kerry, akiwa na Mfalme Abdullah na Benjamin Netanyahu
John Kerry, akiwa na Benjamin Netanyahu na Mfalme AbdullahPicha: Reuters/Y. Allan

Ghasia zimepamba moto wiki za hivi karibuni

Katika wiki za hivi karibuni, ghasia kati ya Israel na Palestina zimepamba moto kwenye mji wa Jerusalem wenye msikiti wa Al-Aqsa, eneo ambalo ni takatifu kwa Waislamu na Wayahudi. Kumekuwa na hofu kwamba ghasia hizo huenda zikachochea kuzuka kwa vuguvugu jipya la Wapalestina.

Siku ya Jumatano, Israel iliidhinisha mpango mpya wa ujenzi wa makaazi ya walowezi, mashariki mwa Jerusalem, licha ya ghasia kuzidi kupamba moto. Hata hivyo, mpango huo umekosolewa vikali na Marekani, Jordan pamoja na Palestina.

Wakati huo huo, Israel imeondoa kizuizi cha umri wa watu wanaotakiwa kwenda kuswali kwenye msikiti wa Al-Aqsa. Msemaji wa Polisi wa Israel, Mickey Rosenfeld, amesema leo kuwa wanaume wa rika zote wataruhusiwa kuhudhuria Swala ya Ijumaa, katika msikiti huo ulioko Jerusalem, ambao umekuwa ukigombaniwa.

Rosenfeld amesema wanategemea kwamba hali itakuwa ya utulivu kutokana na hatua hiyo. Amebainisha kuwa hatua hiyo imefikiwa kutokana na mazungumzo yaliyofanyika Jordan kati ya Kerry, Mfalme Abdullah na Netanyahu. Amesema polisi zaidi wamepelekwa Jerusalem leo asubuhi kwa lengo la kuzuia matukio yoyote yanayoweza kusababisha kuvunjika kwa amani kwenye eneo hilo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,RTRE,AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef