1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yasema inafanya kila juhudi kulinda mipaka yake

13 Aprili 2018

Wanajeshi wa Israel wamewapiga risasi na kuwajeruhi wapalestina zaidi ya 100 wakati wa maandamano makubwa kati ya mpaka wa Israel na Ukanda wa Gaza

https://p.dw.com/p/2w1SX
Proteste in Gaza City
Picha: Getty Images/AFP/M. Hams

Maelfu ya wapalestina waliwasili katika makambi karibu na uzio wakati wa maandamano hayo yaliyopewa jina la "The Great March of Return” yaani maandamano makuu ya kurejea. Maandamano hayo yaliyoingia wiki yake ya tatu sasa yameanzisha tena wito wa wakimbizi kurejea nyumbani ambako ni Israel.

Aidha wanajeshi wa Israel wamewapiga risasi na kuwauwa wapalestina 30 huku mamia kadhaa wakijeruhiwa tangu kuanza kwa maandamano hayo, hatua iliyokosolewa kimataifa juu ya mbinu za hatari zinazotumiwa dhidi ya wapalestina.

Proteste im Gazastreifen
Picha: Reuters/I. A. Mustafa

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pamoja na Umoja wa Ulaya wametoa wito wa kufanyika uchunguzi huru juu ya iwapo wanajeshi wa Israel wanatumia nguvu kupita kiasi kwa waandamani wa Palestina.

Hii leo makundi ya vijana kutoka palestina walipeperusha hewani bendera yao na kuchoma matairi kadhaa pamoja na bedera za Israel karibu na mpaka uliyozingirwa baada ya sala ya Ijumaa. Katika kambi moja Mashariki mwa Ukanda wa Gaza vijana walibeba mabegani sanduku la kubebea maiti lililofunikwa kwa bendera ya Israel likiwa na maneno yaliyoandikwa mwisho wa Israel.

Hata hivyo msemaji wa jeshi la Israel amesema wanajeshi wake wanajibu mashambulizi kutoka kwa waandamanaji wa palestina wanaowarushia mawe na mabomu ya petroli.

Kandoni mwa  hayo Murad Adayleh msemaji wa chama cha Muslim Action Front nchini Jordan amesema anaunga mkono maandamano ya Wapalestina kudai kurejea Israel.

Israel inasema inafanya kila iwezalo kulinda mipaka yake

Israel imewaweka wanajeshi wake kati ya mpaka wake na ukanda wa gaza ili kuwazuwia wapalestina kuingia huko.  Mpaka sasa hakuna muisraeli aliyeuwawa katika maandamano hayo na makundi ya kutetea haki za binaadamuu linasema jeshi la Israel limetumia risasi za moto  dhidi ya waandamanaji. 

Israel Israelische Soldaten im Gazastreifen
Picha: Reuters/A. Cohen

Kwa upande wake Israel imesema inafanya kila juhudi kulinda mipaka yake na kuzuwiya waandamanaji kuingia katika uzio uliyopo.

Maandamano yaliyopangiwa kufanyika kwa wiki sita, yameamsha matakwa ya siku nyingi ya haki ya kurejea wakimbizi wa Palestina katika miji na vijijii ambao familia zao zilitoroka  au kuondolewa wakati taifa la Israel lilipoanzishwa miaka 70 iliyopita. 

Maandamano yalianza tarehe 30 mwezi Machi na yanatarajiwa kumalizika mwezi Mei tarehe 15.

Kwa muongo mmoja sasa Ukanda wa Gaza umezingirwa na wanajeshi wa Israel huku mpaka wake na Misri pia ukifungwa katika miaka ya hivi karibuni.

Mwandishi Amina AbubakarAFP/AP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman