1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina wakabiliana na jeshi la Israel

Mohammed Khelef5 Oktoba 2015

Mpalestina mmoja amekufa kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya makabiliano kati ya waandamanaji na wanajeshi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi, ambako mamia ya wengine wanatibiwa kwa majeraha.

https://p.dw.com/p/1Gidw
Polisi wa Israel akimzuia kijana wa Kipalestina kuingia kwenye Msikiti wa al-Aqsa mwishoni mwa mwezi Septemba 2015.
Polisi wa Israel akimzuia kijana wa Kipalestina kuingia kwenye Msikiti wa al-Aqsa mwishoni mwa mwezi Septemba 2015.Picha: Getty Images/AFP/A. Gharabli

Hudhaifa Suleiman mwenye umri wa miaka 18 alipigwa risasi kifuani hapo jana pale mamia ya Wapalestina walipokabiliana na wanajeshi wa Israel karibu na makaazi ya walowezi wa Kiyahudi kaskani mwa mji wa Tulkarm, Ukingo wa Magharibi. Alifariki dunia kwenye hospitali ya mji huo, licha ya kufanyiwa upasuaji.

Mapigano makubwa yalizuka hapo jana kati ya Wapalestina na wanajeshi wa Israel katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki. Taarifa kutoka hospitali zinasema Wapalestina wapatao 450 walijeruhiwa kwenye mapambano hayo, baadhi yao kwa risasi za moto na wengine za mpira.

Magari matatu ya Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina ambayo yalikuwa yakiwakusanya majeruhi, nayo pia yalishambuliwa, amesema Urab Fuqaha, msemaji wa shirika hilo.

Mamlaka za Israel zimeifunga sehemu ya Mji Mkongwe ya Jerusalem kwa siku mbili zaidi, zikiwazuia Wapalestina kuingia kwenye eneo hilo, ingawa zinawaruhusu walowezi wa Kiyahudi wenye msimamo mkali kuingia kufanya ibada zao.

Msemaji wa polisi ya Israel, Micky Rosenfeld, anasema hatua hiyo inakusudia kuwalinda raia dhidi ya mashambulizi zaidi. "Waisraeli wawili wameuwa ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita mjini Jerusalem kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na Wapalestina. Mji Mkongwe na eneo lote zima limefungwa na askari zaidi wametumwa huko kuzuia mashambulizi zaidi."

Waisraeli wanne wauawa

Polisi ya Israel inasema usiku wa Jumamosi, kijana mmoja wa Kipalestina aliwauwa kwa kuwachoma visu Waisraili hao wawili na masaa machache baadaye, kijana mwengine wa Kipalestina akamchoma kisu mvulana wa miaka 15. Hata hivyo, washambuliaji wote wawili walipigwa risasi na kuuawa na polisi.

Polisi wakiweka vizuizi ya kuingia kwenye sehemu ya mji mkongwe, Jerusalem, siku ya tarehe 3 Oktoba 2015, baada ya raia wawili wa Israel kuuawa kwa kuchomwa visu.
Polisi wakiweka vizuizi ya kuingia kwenye sehemu ya mji mkongwe, Jerusalem, siku ya tarehe 3 Oktoba 2015, baada ya raia wawili wa Israel kuuawa kwa kuchomwa visu.Picha: picture-alliance/Xinhua/Jini

Familia ya mmoja wao, ilisema baadaye kuwa kijana wao hakuwa mshambuliaji, bali mwenyewe alishambuliwa na kundi la Mayahudi wenye msimamo mkali na alipokimbilia kwa polisi akapigwa risasi.

Afisa wa ngazi za juu wa Chama cha Ukombozi wa Palestina, Hannan Ashrawi, ameiita hatua ya Israel kuwazuia Wapalestina kuingia Jerusalem kuwa ni kituko.

"Jerusalem ni mji wa Kipalestina, na sasa Israel inawaambia Wapalestina hao kuwa hawana ruhusa kuingia mji wao wenyewe, wanaufunga mji mkongwe na kuwazuia Wapalestina kuingia, lakini wanawaruhusu na kuwalinda walowezi kuwashambulia Wapalestina kila mahala. Makundi ya siasa kali yanaamua ajenda na hapana shaka serikali yao inatafuta sababu za kuongeza ghasia," alisema mjumbe huyo wa PLO.

Katika hatua nyengine, jeshi la Israel limefanya mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo kadhaa ya Ukanda wa Gaza mapema leo, likidai kujibu maroketi yaliyorushwa na kundi la Hamas.

Israel inasema maroketi 16 yaliyorushwa kutokea Gaza yameangukia sehemu zisizo watu, nayo imeipiga kambi ya Hamas kaskazini mwa Ukanda huo. Hakuna taarifa za waliouawa au kujeruhiwa hadi sasa.

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amerejea nyumbani akitokea Washington na kukutana na baraza lake la usalama, huku Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya zikitoa wito wa pande zote mbili kujizuwia na vitendo vitakavyoifanya hali kuwa mbaya zaidi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga