Wapiga kura barani Ulaya washiriki uchaguzi wa bunge
8 Juni 2024Takriban raia milioni 400 wa Umoja wa Ulaya wanaendelea na zoezi la upigaji kura leo, kuwachagua wajumbe wa Bunge la Ulaya, katika mojawapo ya matukio makubwa ya kidemokrasia duniani.
Vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia vinatafuta kupata uungwaji mkono zaidi katikati mwa ongezeko la gharama za maisha na kutoridhika kwa wakulima. Vita vya Gaza na Ukraine pia ni miongoni mwa masuala yanayojadiliwa mno.
Uchaguzi wa Bunge la Ulaya hufanyika kila baada ya miaka mitano katika jumuiya hiyo yenye wanachama 27.
Uchaguzi huo ulianza Alhamisi wiki hii nchini Uholanzi na utakamilika siku ya Jumapili, wakati nchi nyingi zitakapokamilisha zoezi la uchaguzi. Matokeo ya awali yataanza kutolewa jioni baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa katika nchi zote wanachama.