Wapiganaji kupokonywa silaha huko Palestina
30 Desemba 2007Matangazo
Rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas, ameamuru makundi yote yenye silaha katika ukingo wa magharibi wa mto Jordan yapokonywe silaha.
Rais Abbas ameitangaza amri hiyo baada ya waisraeli wawili kuuwawa hapo Ijumaa iliyopita. Amri hiyo pia inawaathiri wanamgambo wa kundi la Hamas walio katika eneo la Ukanda wa Gaza na wanamgambo wa kundi al Aqsa wa chama Fatah.
Wakati huo huo, kundi la Hamas limeitaka Misri ifungue mpaka wake na eneo la Ukanda wa Gaza ili kuwaruhusu wapalestina 2,000 warejee makwao kutoka hija huko Makkah Saudi Arabia. Mahujaji hao hawataki kurudi kupitia Israel wakihofia kutishwa na wanajeshi wa Israel.