1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa zamani wa asisitiza katiba mpya Tanzania

13 Julai 2021

Vuguvugu la kutaka  mabadiliko ya katiba mpya Tanzania bado liko juu na safari hii, waziri mkuu mstaafu na aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya katiba, Jaji Joseph Warioba ametoa himizo hilo.

https://p.dw.com/p/3wPOG
Kenia Nairobi | Besuch Samia Suluhu Hassan, Präsidentin Tansania
Picha: Shisia Wasilwa/DW

Nchini Tanzania vuguvugu la kutaka  mabadiliko ya katiba mpya bado liko juu na safari hii, waziri mkuu mstaafu na aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya katiba, Jaji Joseph Warioba amejitokeza  na kusisitiza haja ya kuwa na maridhiano yatayosaidia kupatikana kwa katiba mpya.

Hayo yanajiri wakati Rais Samia Suluhu Hassan akisisitiza kuwa ingawa utawala wake unatambua jambo hilo lakini unatoa kwanza kipaumbele katika kukuza uchumi. Hoja ya Warioba aliyeitoa katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni cha jijini Dar es Salaam huenda ikachangiza madai yanayoendelea kuibuliwa na wanasiasa hasa wa upinzani wanashinikiza katiba mpya.

Medani ya siasa imechukua nafasi kubwa katika himizo la katiba mpya.

Tansania Opposition Freeman Mbowe
Kiongozi wa upinzani wa Tanzania, Freeman MbowePicha: Emmanuel Herman/REUTERS

Wanasiasa hao kwa nyakati tofauti wamekuwa wazitolea mwito mamlaka za serikali kufufua mchakato wa katiba hiyo mpya uliokwama tangu mwaka 2014 baada ya kufika katika bunge maalumu la katiba.

Jaji Warioba katika mahojiano hayo ingawa hakubainisha msimamo wa moja kwa moja kuhusu takwa la katiba hiyo mpya, lakini ameashiria haja ya kuendelea na mchakato huo na amewashauri wanasiasa kuwa tayari kukutana na Rais Samia ili kuanzisha majadiliano yatayofungua njia ya kumaliza mkwamo huo.

Licha ya katiba kutajwa ni hitaji la kitaifa linapaswa kuwashirikisha wananchi wa kona zote, hata wanasiasa ndio wanaonekana kulivalia njuga zaidi jambo hilo na madai yao makubwa yanaangukia juu ya kutaka tume huru ya uchaguzi, mshindi wa urais awe ni yule anayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura na matokeo ya uchaguzi wa urais kuhojiwa mahakamani.

Fikra ya kugawika wanasiasa kimtazamo Tanzania.

Kwa upande mwingine, hatua ya Jaji Warioba kutaka wanasiasa kuwa tayari kuanzisha majadiliano na Rais Samia kuhusu hoja zao hizo, baadhi ya wanasiasa na wachambuzi wamegawika katika kulijadili jambo hili. Mathalani, mwanasiasa na mchambuzi wa mambo, Sammy Ruhuza amesema anaepinga suala la katiba mpya anajiweka mbali na wananchi.

Wanasiasa wa upinzani wanadai kuwa katiba ya sasa iliyondikwa mwaka 1977 na baadaye kufanyiwa mabadiliko kadhaa ikiwemo ya mwaka 1992 kuruhusu mfumo wa vyama vingi  inatoa upendelea kwa chama tawala CCM.

Chama hicho tawala ingawa katika ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2015 -2020 iliweka kipengele cha kuendelea na mchakato wa katiba na baadaye kipengele hicho kuondolewa kwenye ilani iliyofuata kimekuwa kikisitiza kuwa katiba ya sasa ni bora na inapendekeza kuendelea nayo.