Warundi wakabiliwa na uhaba mkubwa wa mahitaji ya msingi
27 Agosti 2024Mwaka huo wa 2015, Rais wa Burundi wakati huo, Pierre Nkurunziza alikiuka katiba na kugombea tena muhula wa tatu uongozini, hatua iliyosababisha machafuko makali yaliosababisha vifo vya watu wasiopungua 1,200, huku wengine 400,000 wakikimbia nchi hiyo.
Marekani na Umoja wa Ulaya zilijibu mzozo huo kwa kuliwekea vikwazo taifa hilo lenye takriban watu milioni 13, huku misaada ya maendeleo ikikatizwa.Wafanyabiashara Uganda walia na Burundi kufunga mpaka na Rwanda
Hata hivyo Marekani na Umoja huo wa Ulaya zimerejesha misaada hiyo zikitaja baadhi ya maendeleo ya nchi hiyo katika rekodi yake ya haki za binadamu chini ya mrithi wa Rais Nkurunziza, Rais Evariste Ndayishimiye.
Lakini hii leo hali ni mbaya zaidi, anasema Felix, daktari wa Matana, kijiji kilichoko kilomita 70 kusini magharibi mwa Bujumbura.
Felix amesema awali, walikuwa na uhaba wa bidhaa ambao ulidumu kati ya siku mbili au tatu, lakini sasa wamesubiri kwa wiki mbili na bado hawana tarehe ya kupokea bidhaa hizo.
Huku bidhaa zaidi za kimsingi zikiwa ngumu kupatikana katika maeneo mengi ya nchi, bidhaa chache zilizoko zinauzwa kwa bei ya juu kimagendo.Marekani yaitaka Burundi kuheshimu haki za binaadamu
Andre, kijana anayeishi katika wilaya moja ya shughuli nyingi za kaskazini mwa Bujumbura, anasema milolongo mirefu inashuhudiwa nje ya vituo vya mafuta, rafu za maduka hazina bidhaa na maisha yamekuwa magumu kwa wakazi wa Bujumbura.
Andre ameongeza kuwa inawabidi kutembea umbali wa kilomita kadhaa kila siku kwenda kazini kwasababu hakuna mabasi kutokana na uhaba wa mafuta.
Mkazi mwingine mjini Bujumbura, Gerard mwenye umri wa miaka 60, ambaye anamiliki duka dogo la dawa katikati mwa mji huo, anasema wagonjwa wengi wanafariki dunia kutokana na ukosefu wa matibabu fulani.cGerard anasema, bei za dawa anazoweza kuuza zimepanda sana.
Soma: Mafuriko yasababisha maelfu kukosa makazi Burundi
Kulingana na Benki ya Dunia, asilimia 87 ya wakazi wa Burundi wanaishi chini ya dola 1.9 kwa siku katika nchi ambayo kilimo kinachangia asilimia 40 ya pato la taifa na asilimia 80 ya ajira.
Kampuni ya kimataifa ya bima ya mikopo na usimamizi wa athari ya Coface imesema Burundi ilikuwa na akiba ya fedha za kigeni sawa na miezi 0.7 tu ya uagizaji bidhaa kutoka nje mwezi Desemba 2023, ikionya kuwa uhaba wa fedha za kigeni unasalia kuwa sababu kuu ya wasiwasi.
Ili kujaribu kurekebisha hali hiyo, Burundi ilipunguza vikwazo vya kubadilisha fedha za kigeni mwezi Desemba ili kupunguza pengo kati ya viwango rasmi na vile vya kimagendo.
Katika ripoti yake ya mwezi Julai, Coface imesema bidhaa nyingi huagizwa kwa kiwango cha kimagendo isipokuwa uagizaji wa mafuta, dawa na mbolea ambao unadhibitiwa na serikali, hivyo basi mageuzi yameonekana kuwa na ufanisi wa wastani .
Mchumi mmoja nchini humo amesema uchumi wa Burundi unakabiliwa na mapungufu mengi sana, na kutegemea sana misaada.
Mchumi huyo anasema sekta ambazo zilizalisha fedha za kigeni, iwe kilimo au sekta ya madini, ziko taabani hivi leo. Uhaba wa fedha za kigeni unamaanisha kuwa ni vigumu kuagiza bidhaa kutoka nje.
Alipohojiwa na wabunge kuhusu uhaba huo mapema mwaka huu, waziri mkuu Gervais Ndirakobuca alikiri kuwa hana suluhu la kuwasilisha kwao.
Michel, mtumishi wa umma mjini Bujumbura ameonesha kukata tamaa na kusema amepoteza matumaini ya kuona hali ikiimarika, licha ya ahadi za Rais Evariste Ndayishimiye za siku bora za baadaye.