1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaYemen

Wasaudia wakutana na waasi wa Houthi kutafuta amani Yemen

11 Aprili 2023

Kumekuwa na matumaini ya kupatikana amani nchini Yemen kufuatia mazungumzo kati ya maafisa wa Saudi Arabia na waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran mjini Sanaa.

https://p.dw.com/p/4PtoA
Jemen | Houthi-Führer trifft saudische und omanische Delegationen in Sanaa
Picha: SABA NEWS AGENCY/REUTERS

Balozi wa Saudia nchini Yemen Mohammed bin Al-Jaber amesema ziara yake ya mwishoni mwa wiki katika mji mkuu Sanaa unaodhibitiwa na waasi wa Kihouthi ililenga kuufufua mpango wa kuweka chini silaha na kuanzishwa upya mazungumzo ya kisiasa ili kuumaliza mgogoro wa kivita uliodumu kwa miaka tisa.

Al Jaber alikutana na maafisa wa Houthi mjini Sanaa siku ya Jumapili kwa mazungumzo yaliyohudhuriwa pia na maafisa wa Oman. Ziara hiyo ilijiri wakati mazungumzo kati ya Saudi Arabia na Wahouthi yakishika kasi baada ya ufalme huo kufikia makubaliano na Iran mwezi uliopita kurejesha mahusiano yao ya kidiplomasia. Iran ndiye muungaji mkono mkubwa wa kigeni wa waasi wa Houthi katika vita vya Yemen.

Kiongozi wa Houthi akutana na ujumbe wa Oman mjini Sanaa
Saudia inaongoza juhudi za kupatikana amani YemenPicha: SABA NEWS AGENCY/REUTERS

Al-Jaber aliandika kwenye ukurasa wa Twitter kuwa ziara yake ilikusudiwa kuweka utulivu na kusitisha mapigano, kuunga mkono mchakato wa kubadilishana wafungwa na kutafuta mbinu za kufanyika mazungumzo kati ya pande za Yemen ili kufikia suluhisho endelevu la kisiasa nchini Yemen. Kauli zake ndizo za kwanza kutolewa na Saudi Arabia kuhusu ziara hiyo. Mwanadiplomasia huyo wa Saudia alikutana na Mahdi al-Mashat, mkuu wa Baraza kuu la kisiasa la Houthi, linalotawala katika maeneo yanayokaliwa na waasi nchini Yemen.

Abdul Elah Hajar, ni mshauri wa ofisi ya rais wa utawala wa Wahouthi "Tuna uhakika kwamba mashartii yetu yanapaswa kukubaliwa, na Saudi Arabia inapaswa kuwajibika kikamilifu kwa uchokozi ambao umedumu kwa miaka minane na kutilia maanani damu ya mashahidi, majeraha, hasara ya kiuchumi ya kitaifa na miundombinu, na mali za kibinafsi za raia wetu."

Soma pia: Waoman, Wasaudia na Wahouthi wazungumzia amani ya Yemen

Maafisa wa Yemen na Saudia walisema Saudi Arabia na Wahouthi walifikia rasimu ya makubaliano mwezi uliopita ya kuufufua usitishwaji mapigano ambao muda wake ulikuwa umekamilika Oktoba.

Iran yasema mashambulizi ya Houthi dhidi ya Saudia ni onyo

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ameyasifu mazungumzo hayo akisema ni hatua muhimu itakayosaidia kuutatua mgogoro huo na kupunguza mivutano ya kikanda.

Serikali ya Yemen inayotambulika kimataifa imekaribisha kile ilichokiita juhudi za Saudi Arabia za kuzileta pande zinazozozana nchini Yemen kwenye meza ya mazungmzo ili kufikia makubaliano ya kina ya kisiasa.

Ziara ya Al-Jaber mjini Sanaa imejiri siku chache kabla ya utekelezwaji wa mpango wa kubadilishana wafungwa unaotarajiwa baadae wiki hii. Muafaka huo uliosimamiwa na Umoja wa Mataufa mwezi uliopita, unahusisha kuwachiwa kwa karibu wafungwa wa kivita 900 kutoka pande zote, wakiwemo wanajeshi wa Saudia.

Soma pia: Oman yaendeleza upatanishi Wahouthi, Saudi Arabia, Iran

Mzozo wa Yemen ulianza mwaka wa 2014 wakati Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran walikamata Sanaa na upande wa kaskazini mwa Yemen, na kuiondoa serikali inayotambulika kimataifa amabyo ilikimbilia kusini na kisha uhamishoni nchini Saudi Arabia.

Hatua hiyo ya Wahouthi ilipelekea muungano wa kijeshi ukiongozwa na Saudia kuingilia kati miezi kadhaa baadae katika jitihada za kurejesha madarakani serikali iliyotambulika kimataifa. Mzozo huo umegeuka kuwa vita vya wakala kati ya Saudi Arabia na Iran.

AP/AFP