Msako wa washambuliaji wa Charlie Hebdo waendelea
8 Januari 2015Hali ya wasiwasi imezidi kutanda nchini Ufaransa huku serikali ikitangaza leo kuwa siku ya maombolezo baada ya mauaji hayo ya jana. Waziri Mkuu wa Ufaransa, Manuel Valls, amesema washukiwa wa mashambulizi hayo wametambuliwa na maafisa wa ujasusi kuwa ni ndugu wawili, Cherif na Said Kouachi.
Cherif, mwenye umri wa miaka 32, anatuhumiwa pia kwa kukusanya wapiganaji wa jihadi kwa ajili ya kwenda Iraq na pia kukutwa na mwaka 2008 alikutwa na hatia ya ugaidi.
“Yeye pamoja na kaka yake wanapaswa kuchukuliwa kama watu hatari," ilisema polisi ya Ufaransa.
Msemaji wa Ofisi ya Mwendesha Mashitaka mjini Paris, Agnes Thibault-Lecuivre, amesema mshukiwa wa tatu, Mourad Hamyd, mwenye umri wa miaka 18, amejisalimisha mwenyewe polisi katika kijiji kimoja mashariki mwa Ufaransa, baada ya kugundua kuwa jina lake lilikuwa miongoni mwa washukiwa wa mashambulizi waliotangazwa katika mitandao ya kijamii na hata vyombo vya habari.
Hata hivyo, Agnes hakusema mshukiwa huyo alikuwa na mahusiano ya aina gani na kaka hao wawili wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya jana.
Hali ya hadhari yaimarishwa
Kwa sasa Ufaransa imeongeza tahadhari dhidi ya ugaidi na kuimarisha usalama kwenye maeneo kadhaa, ambapo zaidi ya wanajeshi 800 wanashika doria katika ofisi tofauti za vyombo vya habari, maeneo ya kuabudu, maeneo ya usafiri na maeneo mengine yaliyoko katika hatari ya kushambuliwa.
Kumekuwa na taarifa za misikiti kushambuliwa na makundi ya waandamanaji wanaodai kulipiza kisasi mauaji ya jana.
Kumekuwa pia na taarifa za mashambulizi mengine dhidi ya polisi kusini mwa Ufaransa, ambako watu waliokuwa kwenye gari wamewapiga risasi polisi wawili na kumuua mmoja wa kike. Hakuna ushahidi wa kuyaunganisha matukio mawili hayo hadi sasa.
Huku hayo yakiarifiwa raia nchini Ufaransa wanatarajiwa kunyamaa kimya kwa dakika moja mchana wa leo ili kuwakumbuka wahanga wa mashambulizi ya hapo jana, ambapo waandishi wanane wa habari, maafisa wawili wa polisi, mfanyakazi mmoja na mgeni aliyetembelea ofisi hiyo waliuwawa.
Dunia yaungana na Ufaransa
Kwa upande mwengine, viongozi kadhaa duniani wameendelea kulaani mashambulizi hayo. Rais Barrack Obama wa Marekani amesema nchi yake itasimama na Ufaransa katika wakati huu mgumu, huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, akisema mashambulizi hayo "yanaiingilia demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari."
Naye Waziri Mkuu wa Australia, Tony Abbott, ameyalaani mashambulizi hayo na kuyaelezea kama kitendo cha ukatili wa hali ya juu, huku Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameroon akisema Uingereza iko pamoja na Ufarasa dhidi ya ugaidi na dhidi ya kitisho cha maadili wanayoyalinda, uhuru wa kujieleza pamoja na demokrasia.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga