1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Bush atishia vikwazo zaidi kwa Myanmar

16 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7FT

Rais George W. Bush wa Marekani ameitaka jumuiya ya kimataifa kuzidi kuushinikiza utawala wa kijeshi wa Myanmar.

Rais Bush hapo jana ametishia kuuwekea utawala huo vikwazo zaidi lakini amesema vikwazo hivyo havitokuwa na maana iwapo Marekani itakuwa nchi pekee inayoweka vikwazo.Mjini Washington msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Tom Casey amezitaka China,India na mataifa mengine ya Asia kutumia ushawishi wao kuilazimisha serikali ya Myanmar kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa na kuwa na mazungumzo na upinzani baada ya kuvunja kwa kutumia nguvu maandamano ya kudai demokrasia nchini humo.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Myanmar Ibrahim Gambari yuko ziarani barani Asia kwa dhamira hiyo hiyo na wakati akiwa Bangkok nchini Thailand hapo jana amesema repoti za kukamatwa kwa viongozi wa wanafunzi waliobakia,mateso na vitendo vya vitisho ni mambo ya usumbufu mkubwa sana na yanakwenda kinyume na mazungumzo ya pande mbili kati ya Umoja wa Mataifa na Myanmar.Vitendo hivi lazima vikome mara moja.

Hapo jana mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya pia waliidhinisha vikwazo vipya dhidi ya serikali ya Myanmar ikiwa ni pamoja na kususia usafirishaji kutoka nchi hiyo wa mbao,vito vya thamani na metali.