Washington. Marekani yafikiria kuiondolea vikwazo vya biashara na kiuchumi Sudan.
25 Juni 2005Waziri wa mambo ya kigeni wa Sudan Mustafa Osman Ismail amesema jana kuwa waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice amekubali kuangalia uwezekano wa kuondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya taifa hilo la kaskazini mashariki ya Afrika.
Akizungumza baada ya mazungumzo na wanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani , amesema kuwa matatizo makubwa ambayo yamekuwa kikwazo kwa uhusiano wa kawaida kati ya mataifa hayo mawili yameondolewa na kwamba amemtaka Bibi Rice kuondoa vikwazo hivyo vya biashara na uchumi.
Amedai kuwa masharti yaliyowekwa dhidi ya serikali ya Sudan ili kuweza kuondoa vikwazo hivyo ni kumalizika kwa ghasia katika jimbo la Dafur na mzozo uliodumu kwa muda wa miaka 20 upande wa kusini mwa nchi hiyo pamoja na nchi hiyo kutoa ushirikiano kwa Marekani katika vita vyake dhidi ya ugaidi.