Washirika wa Nato wageuka maadui
2 Agosti 2018Mgogoro huu wa kidiplomasia unatokana na kisa cha kushikiliwa mchungaji mmoja wa Kimarekani nchini Uturiki kwa tuhuma za kuhusika na ugaidi.
Hali ya wasiwasi na mivutano imeongezeka wiki za hivi karibuni kufuatia hatua ya Uturuki ya kumuweka kizuizini kwa tuhuma za ugaidi mchungaji Andrew Brunson raia wa Kimarekani ambaye alifungwa jela kwa mara ya kwanza Oktoba mwaka 2016 na baada ya kuachiliwa aliwekwa tena katika kizuizi cha nyumbani wiki iliyopita. Mahakama inayosikiliza kesi ya Brunson mara kadhaa imepinga kuachiwa huru kwa mchungaji huyo ambaye atarudishwa tena mahakamni Oktoba 12. Hatua ya kuwekwa katika kifungo cha nyumbani dhidi ya mchungaji Brunson ambaye akiliongoza kanisa la kiprotestanti katika mji wa Izmir iliibua mivutano zaidi badala ya kutuliza hali ya mambo ambapo rais Donald Trump na makamu wake Mike Pence waliionya Uturuki kwamba itakabiliwa na vikwazo.
Vikwazo hivyo sasa vimetangazwa vikiwalenga waziri wa sheria Andulhamit Gul na waziri wa mambo ya ndani Suleyman Soylu ambapo Marekani imetangaza kuzizuia akaunti zao au mali zao zozote katika ardhi ya nchi hiyo huku pia raia wa Marekani wakizuiwa kufanya bishara ya aina yoyote na maafisa hao wa ngazi ya juu wa Uturuki. Wizara ya fedha ya Marekani imetowa taarifa jana ikisema kwamba maafisa hao waliowekewa vikwazo ni viongozi katika serikali ya Uturuki wanaohusika na utekelezaji wa vitendo vibaya vya ukiukaji wa haki za binadamu.
Msemaji wa ikulu ya Marekani Sarah Sanders pia alitoa taarifa mbele ya waandishi habari akieleza kwamba mawaziri wote wawili wamekuwa na dhima kubwa katika hatua ya kumkata na kumfunga mchungaji Brunson. Kufutia kishindo hicho kutoka Marekani Uturuki nayo imeghadhabika,wizara yake ya mambo ya nje imeshaonya kwamba hatua ya Marekani itaharibu kabisa juhudi za ufanisi za kuyatatua masuala kadhaa yaliypo kati yake na Marekani na kusisitiza kwamba Uturuki italipiza kisasi bila kuchelewa.
Rais Recep Tayyip Erdogan ambaye anajiandaa kuongoza mkutano wa baraza kuu la kijeshi la Uturuki bado hajatowa kauli yoyote kuhusu hatua hii mpya ya Marekani ingawa jana aliapa kwamba katu hatopiga magoti na kusifia vitisho kutoka Marekani ambayo ameishutumu kwa kuonesha kile alichokiita mtazamo wa kiinjilisti na kizayuni. Mvutano huu unaonekana kuwa mmoja wa mivutano mikubwa kuwahi kutokea kati ya Marekani na Uturuki katika historia ya Uturuki ya sasa tangu ulipotokea ule mvutano wa 1974 baada ya Uturuki kuivamia Cyprus na upande mwingine Marekani ilipoivamia Iraq 2003.
Brunson anatuhumiwa kuwa jaasusi anayefanya kazi kwa niaba ya makundi mawili yanayotajwa na Uturuki kuwa ya kigaidi,vuguvu linaloongozwa na ulamaa wa kiislamu Fethullah Gulen anayetuhumiwa na Uturuki kuwa nyuma ya jaribio la mapinduzi la 2016 pamoja na kundi la wafanyakazi wa kikurdi PKK.Kishindo cha mvutano humo kimeiathiri pia thamani ya sarafu ya Uturuki Lira ambapo imeteremka na kufikia kiwango cha dolla moja kubadilishwa kwa Lira zaidi ya 5.
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri: Josephat Charo