Washirika wa Somalia waelezea wasiwasi wa mzozo wa kisiasa
28 Desemba 2021Wanajeshi watiifu kwa waziri mkuu Mohammed Hussein Roble walijikusanya karibu na ikulu ya rais, siku moja baada ya Rais Mohamed Abdullahi Momahed, maarufu kama Farmajo, kutangaza kutimuliwa kwa Roble, ambaye alimtuhumu kwa kufanya njama ya jaribio la mapinduzi.
Waangalizi wa kimataifa na washirika, ukiwemo Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani nchini Somalia – AMISOM, Marekani, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa, walitoa taarifa jana usiku wakielezea wasiwasi kuhusu mzozo huo.
Soma pia: Roble aviagiza vikosi vya usalama kuchukua amri kutoka kwake
Taarifa hiyo iliwataka viongozi wa Somalia kuyaweka mbele maslahi ya nchi, kuituliza mivutano ya kisiasa inayoongezeka, na kujiepusha na uchochezi au matumizi ya nguvu ambavyo vinaweza kuhujumu amani na utulivu.
Farmajo anamtuhumu Roble kwa kuingilia uchunguzi kuhusu kesi ya unyakuzi wa ardhi na akaondoa mamlaka yake ya kuandaa uchaguzi. Roble naye anamtuhumu Farmajo kwa kujaribu kufanya mapinduzi dhidi ya serikali, katiba, na sheria za nchi na kuuhujumu uchaguzi. "Kama tunavyofahamu, Mohamed Abdullahi Farmaji ni mgombea wa uchaguzi wa rais. Hayuko tofauti na wagombea wengine wa urais. Ninatangaza wazi kwa Farmajo, wewe ni mgombea, simama pembeni, kama walivyo wagombea wengine na ugombee kiti hicho, kwa hiyo wanajeshi hawawezi kufuata amri ya Farmajo na hawezi kuwaamuru." Amesema Roble.
Mahusiano kati ya viongozi hao wawili kwa muda mrefu yamekuwa mabaya, lakini matukio ya karibuni yamezusha wasiwasi kwa utulivu wa Somalia wakati nchi hiyo inajitahidi kuandaa uchaguzi uliocholeweshwa muda mrefu na kupambana na uasi wa itikadi kali.
Kando na waangalizi wa kimataifa, baadhi ya wazee wa kimila na wanasiasa wamejaribu kutuliza joto. Chanzo kutoka ofisi ya rais kimeliambia shirika la habari la AFP kuwa juhudi za wazee hao bado hazijapata ufumbuzi rasmi. Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani inayohusika na masuala ya Afrika imeonya kuwa Washington imejiandaa kuchukua hatua dhidi ya wale wanaozuia njia ya amani nchini Somalia.
Wachambuzi wanasema mkwamo wa uchaguzi unayafunika matatizo makubwa ya Somalia na hasa uasi wa kundi la al-Shaabab.
Washirika hao wa al-Qaeda walifurushwa Mogadishu muongo mmoja uliopita lakini wakachukua tena udhibiti wa maeneo ya mashambani na wanaendelea kufanya mashambulizi makali katika mji mkuu na kwingineko.
AFP