Washukiwa wakamatwa Pakistan baada ya shambulio
29 Machi 2016Waziri wa sheria wa jimbo la Punjab Rana Sanaullah amewaambia waandishi wa habari Jumanne(29.03.2016) kwamba zaidi ya watu 5,000 walihojiwa na kupekuliwa na wengi wao waliachiliwa baadae lakini wengine 216 wanaendelea kushikiliwa kwa uchunguzi zaidi.
Mamia walijeruhiwa wakati miripuko iliyotegeshwa miongoni mwa ummati mkubwa wa watu iliporipuliwa na mshambuliaji wa kujitowa muhanga karibu na uwanja wa kuchezea watoto shambulio linalodaiwa kufanywa na Jamat -ul- Ahrar ambacho ni kitengo cha kundi la Tehrrek- i- Taliban Pakistan (TTP).
Msemaji wa kitengo hicho amesema walikuwa wamewalenga Wakristo.
Kwa mujibu wa Sanaullah operesheni 56 za kijasusi zimetekelezwa na polisi kwa kushirikiana na wanamgambo, majeshi na mashushu wa ujasusi katika kipindi cha masaa 24 kwenye jimbo hilo la Punjab.
Kupambana na ugaidi hadi kieleweke
Katika hotuba kwa taifa iliyoonyeshwa na televisheni hapo Jumatatu Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Shariff ameahidi tena kupambana na ugaidi kufuatia miripuko ya Jumapili katika mji mkuu wa jimbo la Punjab wa Lahore.
Amekaririwa akisema "Leo nimeamuwa kuja kwenu kurudia kiapo changu kwamba tunahesabu kila mtu aliyepoteza maisha na kila tone la damu lililomwagwa na watu waliokufa wakiwa mashahidi.Kisasi hiki kitalipizwa na hatutopumuwa hadi hapo sehemu ya mwisho ya mahesabu ya kisasi itakapomalizika."
Takriban watoto 29 waliokuwa wakifurahia Pasaka mwishoni mwa juma ni miongoni mwa watu waliouwawa wakati mripuaji alipojiripuwa kwenye bustani mashuhuri iliojaa harakati mjini Lahore ambayo ni ngome kuu ya Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Shariff.
Shariff akejeliwa
Wanamgambo wa Taliban wamemkejeli Shariif katika mtandao wa Twittrer kwa kusema kwamba vita walivyotangaza sasa vimefika mlangoni kwa Shariff na kwamba Mungu akipenda mujahideen watashinda vita hivyo.
Pakistan ni nchi yenye idadi kubwa ya Waislamu lakini Wakristo walioko nchini humo wanafikia milioni mbili.
Msako wa kuwatafuta wanamgambo waliohusika na shambulio hilo unaendelea katika jimbo hilo la Punjab ambalo ndio jimbo tajiri kabisa na lenye idadi kubwa ya watu nchini Pakistan.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/
Mhariri : Iddi Ssessanga