Wasiwasi wa kufanyika mkutano wa Korea mbili
23 Mei 2018Tukio hilo linaangaliwa kuwa ni hatua njema kuelekea mkutano wa kilele unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao, kati ya rais Donal Trump wa Marekani na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, licha ya shaka shaka ziliopo. Kuharibiwa kwa eneo hilo la majaribio ya nyuklia kunatarajiwa kufanyika kati ya leo Jumatano na Ijumaa, ikitegemea hali ya hewa. Korea Kaskazini inaichukulia hatua yake hiyo kuwa ni ya moyo mwema, kabla ya mkutano huo wa kilele uliopangwa kufanyika Juni 12 nchini Singapore.
Mashaka ya kufanyika mkutano wa kilele wa Korea Kaskazini na Kusini
Lakini pande zote mbili zimeelezea shaka shaka iwapo kweli mkutano huo wa kihistoria utafanyika. Korea Kaskazini ilitishia kujiondoa ikiwa Marekani itaishinikiza iachane na shughuli zake za kinyklia. Pia Trump alisema baada ya kukutana na Rais wa Korea Kusini Moon Jae-In jana Jumanne mjini washington, kwamba mkutano wake na Kiongozi wa Korea Kaskazini unaweza ukacheleweshwa. Baadaye aliwaambia waandishi habari kwamba Kuna masharti fulani ambayo Marekani inataka yatimizwe. Alisema anafikiri masharti hayo yatatekelezwa la sivyo hapatokuweko na mkutano unaotarajiwa. Trump hakufafanua juu ya masharti hayo.
Jitihada za Trump za kukutana na Kim Jong Un
Kisiasa Trump amefanya juhudi kubwa ili mkutano wake wa kilele na Kim ufanikiwe, na faraghani maafisa wa marekani na pia waangalizi wa kigeni wanaamini utafanyika kama ulivyopangwa. Lakini wakati siku zikizidi kusogea kuelekea Juni 12, kuna hali ya wasiwasi na tafauti zilizopo kati ya pande hizo mbili zinazidi kujitokeza. marekani imeeleza wazi inataka Korea Kaskazini iachane na shughuli zake za kinyklia, na Korea kaskazini imekula kiapo kwamba haitofanya hivyo hadi ina uhakika iko salama kutokana na kile inachokiona kuwa ni uchokozi wa Marekani. Awali waandishi habari kutoka Korea Kusini waliachwa nyuma kwa kuwa hawakupata kibali kutoka PyongYang. Hata hivyo Wizara ya Korea Kusini inayohusika na suala la muungano wa korea mbili, ilisema waandishi hao sasa wameruhusiwa, kushiriki katika dakika ya mwisho.
Waangalizi watashuhudia kuharibiwa kwa eneo la majaribio ya Kinyuklia. Wakosoaji wanasema eneo hilo tayari halina maana baada ya kutumiwa kwa majaribio 6 hapo kabla , hata hivyo ikihitajika linaweza kuandaliwa kwa majaribio mengine. Waandishi habari kutoka China, marekani na Urusi walisafiri kwa ndege ya kukodi jana kutoka Beijing hadi mji wa Korea kaskazini wa Wonson. Kutoka huko wanatarajiwa kusafiri kwa muda wa masaa 20 kwa treni na basi hadi mwambao wa mashariki.
Wakati hayo yakijiri , Wizara ya mambo ya nchi za nje ya China , imesema leo kwamba nchi hiyo imetoa mchango mkubwa katika rasi ya Korea na inamatumaini mkutano wa kilele kati ya Marekani na Korea Kaskazini unaweza kufanyika. taarifa ya Wizara hiyo ilitolewa katika kikao cha kawaida na waandishi habari. Jana Rais Trump wa Marekani alirejea tena matamshi yake kwamba anafikiri mkutano wa karibu kati ya Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un na rais Xi Jinping wa China ulimshawishi Kim kuwa na msimamo mkali kabla ya mkutano wake na Trump.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, afp rtr
Mhariri: Iddi Ssessanga