Wasiwasi watawala tena Ukraine Mashariki
4 Juni 2015Msemaji mkuu wa jeshi la Ukraine, Andriy Lysenko amesema leo kuwa wanamgambo 80 wanaoelemea upande wa Urusi wameuwawa na 100 wengine kujeruhia kufuatia kushindwa jaribio lao la kuvamia maeneo yanayodhibitiwa na serikali ya Ukraine.
Mapigano hayo yalitokea jana kusini-magharibi mwa Ukraine nje kidogo na mji wa Donetsk ambao ndio ngome ya waasi, baada ya serikali ya Ukraine kuwashutumu wanamgambo hao kufanya mashambulizi katika mji wa of Maryinka.
Rais wa Ukraine Petro Poroshenko ameonya juu ya hatari ya Ukraine kuvamiwa na Urusi katika hotuba yake kwa bunge, na kusema kuna zaidi ya wanajeshi 9,000 wa Kirusi ndani ya Ukraine ambao ni tishio kubwa la kuzuka tena vita nchini humo.
"Wakati huo huo, bado tishio la vita na makundi ya kikaidi ya Urusi limebaki kuwepo. Katika ardhi ya Ukraine, kuna zaidi ya makundi 14 ya kimkakati ya Urusi na idadi kamili ya wanajeshi hao ni zaidi ya 9,000. Idadi ya wanajeshi wa Urusi karibu na mpaka wa Ukraine imezidi zaidi ya nusu ya ile ya mwaka jana.”
Katika mkutano na waandishi habari mjini Kiev, Lysenko amesema pia wanajeshi watano wa Ukraine wameuawa katika mapigano hayo ambayo ni mabaya zaidi tangu kusainiwa kwa makubaliano ya kusitishwa kwa mapigano mnamo mwezi wa Febuari.
Mapigano yakiuka makubaliano ya Minsk
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami NATO Jens Stoltenberg amesema Urusi ina jukumu la kuhakikisha kuwa hakuzuki vita upya Mashariki mwa Ukraine.
Naye waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na mwenzake wa Ukraine Pavlo Klimkin, alisema katika mkutano na waandishi habari kuwa Ujerumani ina wasiwasi mkubwa juu ya kukiukwa kwa makubaliano ya Minsk yaliyozitaka pande hizo mbili kusitisha mapigano.
"Mapigano ya jana yana hatari ya kurejesha tena vita nchini humo, hilo lazima lizuiliwe kutokea," alisema Steinmeier.
Naye balozi wa Ukraine kwa Umoja wa Ulaya, Kostiantyn Yelisieiv, imeusisitizia umoja huo kuchukua hatua za mara moja za kuengeza vikwazo ilivyoiwekea Urusi kufuatia mapigano hayo mapya.
Yelisieiv ameyaita mapigano hayo yaliyotokea jana kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa makubaliano ya Minsk, ya kusitisha mapigano yaliyosainiwa mwezi wa Febuari chini ya usimamizi wa Umoja wa Ulaya.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya walikubaliana mwezi Machi kuwa vikwazo dhidi ya Urusi, vitabaki kuwepo hadi makubaliano ya Minsk yatekelezwe kikamilifu na kuipa Urusi hadi mwisho wa mwaka huu.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpae,rtre,ape,afpe.
Mhariri:Iddi Ssessanga