Wasoshalisti washinda tena Ufaransa
18 Juni 2012Ni hali ya furaha mbele ya makao makuu ya chama cha kisoshalisti mjini Paris. Mwenyekiti wa chama hicho, Martine Aubry, anazungumza mbele ya Televisheni. Anayataja matokeo hayo kuwa ni heshima kubwa na pia wajibu mkubwa.
"Wafaransa wamebainisha wazi kwamba wanataka mabadiliko ya kisiasa yaliyoanza na uchaguzi wa rais na yatazidi kuendelea," alisema Aubry. Kwa mujibu wa matokeo ya mwanzo, Chama cha Kisoshalisti na washirika wake wamepta viti kati ya 308 na 320 kati ya viti 577.
Kwa matokeo haya, wasoshalisti sasa wana nguvu isiyo kifani, baada ya kushinda urais, mabraza yote mawili ya bunge na mikoa mingi zaidi na miji mikubwa. Matokeoa haya pia yanaimarisha nafasi ya rais Hollande si tu nchini Ufaransa, bali pia katika kanda inayotumia sarafu ya euro.
Ushindi unatoa changamoto kubwa
Lakini Waziri Mkuu wake, Jean-Mark Ayrault, alisita kusherehekea ushindi huu, akisema serikali yake inakabiliwa na jukumu zito, hasa kwa kuzingatia hali ngumu ya kiuchumi inayolikabili bara la Ulaya: "Sasa tuko katika nafasi ya kuanza kuifufua Ufaransa na kuiacha itoe haki. Kwa wingi huu tuliyoupata katika Bunge, tunaweza kutatua matatizi yetu sasa."
Wakati huo huo, chama cha kihafidhina cha rais wa zamani wa nchi hiyo, Nicolas Sarkozy kiliendelea kupoteza viti, kwa kupata kati ya viti 212 na 221 kutoka viti 304 kilichokuwa na vyo katika bunge lililopita. Kiongozi wa chama hicho cha UMP, Jean-Francois Cope, alitambua ushindi wa wasoshalisti na kuomba kuwepo na umoja ndani ya chama chake.
Nacho chama chenye msimamo mkali cha mrengo wa kulia - National Front- kilifanikiwa kupata viti viwili baada ya kutokuwa bungeni kwa miongo miwili, huku naibu wa kiongozi wa chama hicho, Marion Marechal-Le Pen, akichaguliwa kuwakilisha mkoa wa kusini wa Carpentras. Lakini mambo yalikuwa tofauti kwa kiongozi wa chama hicho, Marine Le Pen, aliepoteza kwa mgombea wa Kisoshalsti kaskazini mwa Ufaransa.
Apinga matokeo, kukata rufaa
Le Pen, hata hivyo, amepinga matokeo hayo na kusema kuwa atakata rufaa katika baraza la katiba kutaka kurudia kuhesabu kura hizo ambazo zinaonyesha alishindwa kwa kura 118 na msoshalisti Philippe Kemel.
Ushindi wa wasoshalisti ni wa kustajaabisha ikizingatiwa kuwa chama hiki kilikuwa kinabiliwa na migawanyiko katika muongo uliyopita, kisijue wapi pa kuelekea. Ushindi huo mnono ni zaidi ya viti 289 vinavyotakiwa kuwa na wingi wa kufanya maamuzi ,na hii inamaanisha kuwa hawatahitaji kuungwa mkono na wasoshalisti wenye msimamo mkali ambao wanapinga baadhi ya sera za chama hicho zinazoegemea zaidi Umoja wa Ulaya.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\APE\DPAE
Mhariri: Othman Miraji