Wasyria wa maeneo yanayodhibitiwa na serikali wanapiga kura
26 Mei 2021Zaidi ya watu milioni 18 wana haki ya kupiga kura ndani na nje ya Syria kulingana na Waziri wa Mambo ya Ndani Mohammed al Rahmoun.
Ameongeza kuwa jumla ya vituo 12,102 vya kupigia kura vimeandaliwa. Lakini sio wapiga kura wote waliojiandikisha watakaoweza wakajitokeza, kwani taifa hiyo bado limetawaliwa na vurugu.
Mgogoro wa Syria ulioanza 2011, umesababisha vifo vya watu 400,000 na kupelekea nusu ya idadi ya watu wa nchi hiyo kabla ya kuzuka vita kupoteza makazi yao kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa.
Kwa msaada wa Iran na Urusi, al-Assad ameweza kuchukua tena udhibiti wa zaidi ya asilimia 60 ya nchi. Waasi bado wanashikilia maeneo kadhaa kaskazini na kaskazini magharibi mwa Syria, wakati Wakurdi wanatawala maeneo ya kaskazini mashariki.
Al-Assad, mwenye umri wa miaka 55 anatarajiwa kushinda muhula wa nne wa miaka saba katika uchaguzi wa leo ambao upinzani umeutaja kuwa ni wa undanganyifu.
Wagombea watatu wa urais waidhinishwa na mahakama
Mahakama Kuu ya Kikatiba ya Syria imeidhinisha wagombea watatu ikiwa ni pamoja na Assad katika kinyang'anyiro hicho cha kugombea urais.
Wawili wengine ni Abdullah Salloum, waziri wa zamani, na Mahmoud Marai, kiongozi wa upinzani kutoka mjini Damascus.
Vyama vya upinzani pamoja na wa shirika wao wa nchi za magharibi mara kwa mara vimekuwa vikimtaka Assad kuachia ngazi kama hatua ya kwanza ya kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Usiku wa kuamkia leo siku ya kura, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Uingereza, na mawaziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Ujerumani, na Italia walitoa taarifa ya pamoja ya kulaani uchaguzi huo na kuutaja kuwa ni wa udanganyifu.
Mataifa hayo matano yamesema yanaunga mkono sauti za watu wote wa Syria, ikiwa ni pamoja na asasi za kiraia na vyama vya upinzani ambavyo vimesema mchakato wa kuandaa uchaguzi haukuwa wa halali.
Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa moja asubuhi na kufungwa saa moja usiku kulingana na vyanzo vya serikali ya Syria.
Vyanzo: (dpa, afp)