1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataalamu wa silaha za kemikali kuingia Douma

17 Aprili 2018

Shirika la habari la serikali ya Syria limeripoti kwamba mfumo wa kujikinga na makombora wa nchi hiyo umezuia uvamizi kwa kuyaangusha makombora katika eneo la kati la Homs mapema Jumanne.

https://p.dw.com/p/2wAjH
Niederlande OPCW-Sondersitzung zu mutmaßlichem Giftgaseinsatz in Duma
Picha: picture alliance/dpa/ANP/Evert-Jan Daniels

Shirika la habari la serikali ya Syria limeripoti kwamba mfumo wa kujikinga na makombora wa nchi hiyo umezuia uvamizi kwa kuyaangusha makombora katika eneo la kati la Homs mapema Jumanne. Mashambulizi haya yanakuja mnamo wakati maafisa wa Urusi wamesema wataalamu wa silaha za kemikali wanatarajiwa kuwasili Douma Jumatano kuchunguza madai ya shambulizi la sumu. Wakati huo huo Marekani nayo imeelezea wasiwasi wake kwamba huenda ikawa Urusi tayari imeshaharibu ushahidi katika eneo la tukio.

Ripoti hazikusema ni nani aliyetekeleza mashambulizi hayo ya Jumanne alfajiri ila shirika hilo la habari la serikali limesema makombora hayo yalikilenga kituo cha kijeshi cha Shayrat kilichoko mjini Homs.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Marekani, Ufaransa na Uingereza kufanya mashambulizi ya angani wakilenga sehemu zinazodaiwa kuwa na silaha za kemikali nchini Syria. Mashambulizi haya yalikuwa ni jawabu kwa shambulizi la kemikali ambalo nchi hizo zilidai lilitekelezwa na serikali ya Syria.

Ziara ya wataalamu wa OPCW inapangiwa Jumatano

Kufuatia mashambulizi hayo yaliyofanywa mwishoni mwa juma lililopita kulizuka malumbano makubwa kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi hapo jana. Marekani, Uingereza, Ufaransa na Urusi zilikabiliana vikali kwenye mazungumzo ya dharura katika makao makuu ya shirika la kupambana na matumizi ya silaha za kemikali mjini The Hague, Uholanzi wakati ambapo wachunguzi wanajiandaa kwa kazi ngumu na hatari ya kufanya uchunguzi.

Syrien Luftangriffe auf Ghouta
Serikali ya Syria inatuhumiwa kufanya shambulizi la sumu DoumaPicha: picture-alliance/AP Photo/Syrian Civil Defense White Helmets

Afisa katika Wizara ya Ulinzi ya Urusi Igor Kirillov alizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo wa The Hague. "Tunapanga ziara ya wataalamu wa OPCW ifanyike siku ya Jumatano kwa hiyo Urusi haizuii wachunguzi wa kimataifa kuzuru Douma kwa njia yoyote ile," alisema Kirillov.

Marekani imeilaumu Urusi kwa kuwazuia wachunguzi hao kufika katika eneo kulikofanywa shambulizi linalodaiwa kuwa la kemikali na imesema huenda ikawa Urusi au Syria zimeharibu ushahidi tayari.

Balozi wa Urusi katika shirika la OPCW Alexander Shulgin aliyakanusha madai hayo na kusema nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani hazitaki uchunguzi kwa kuwa zimeshafanya maamuzi yao wenyewe.

May na Macron wamekosolewa na wapinzani wao wa kisiasa

"Labda wanaogopa kwamba baada ya wataalamu hao kufanya uchunguzi wao watapinga kwamba kulikuwa na shambulizi la sumu jambo ambalo lilikuwa kisingizio cha mashambulizi yaliyofanywa na Marekani," alisema Shulgin, "Uingereza na Ufaransa dhidi ya Syria ambayo haikuweza kujitetea," aliongeza balozi huyo wa Urusi.

UK Theresa May im Unterhaus
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ajitetea mbee ya bungePicha: picture alliance/AP Photo/PA

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wamekosolewa na wapinzani wao wa kisiasa kutokana na maamuzi yao ya kushiriki katika mashambulizi dhidi ya Syria. Lakini May alijitetea mbele ya bunge na kupata uungwaji mkono kwa uamuzi wake.

"Wacha niwe muwazi kabisa. Tumeshambulia kwasababu ni jukumu letu la kitaifa. Ni jukumu letu la kitaifa kuzuia kutumika kwa silaha za kemikali nchini Syria na kulinda maelewano ya dunia nzima kwamba silaha hizi hazistahili kutumika," alisema May. "Hatuwezi kukubali silaha za kemikali kufanywa kuwa jambo la kawaida iwe ni nchini Syria, katika mitaa ya Uingereza au mahali kwengine kokote duniani," aliongeza kiongozi huyo wa Uingereza.

Syria na Urusi zinakanusha kutumia silaha za sumu katika mashambulizi yake Aprili 7 mjini Douma yaliyopelekea kuuteka mji huo uliokuwa ngome ya mwisho ya waasi.

Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/APE/AFPE

Mhariri: Iddi Ssessanga