1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia amwaga sifa kwa Mzee Mwinyi, atafuata nyayo zake

2 Machi 2024

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema ataendelea kuyaenzi maono ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Hayati Ali Hassan Mwinyi kwa kusimamia ustawi wa wananchi, kutenda haki na kuwa mstahamilivu.

https://p.dw.com/p/4d6b2
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na mwenzake wa Zanzibar Hussein Mwinyi wakitoa heshima zao za mwisho kwenye jeneza la rais wa zamani wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na mwenzake wa Zanzibar Hussein Mwinyi wakitoa heshima zao za mwisho kwenye jeneza la rais wa zamani wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi.Picha: Zanzibar State House

Rais Samia amesema hayo katika mazishi ya kitaifa ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Hayati Ali Hassan Mwinyi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Michezo wa Amani Abeid Karume.

Aidha, Rais Samia amesema kwa ustahamilivu wake wakati wa uongozi, hayati Mwinyi aliheshimu haki za binadamu na utawala bora na kuruhusu maoni tofauti yenye kuikosoa serikali.

Vile vile, Rais Samia amesema licha ya Hayati Mwinyi kuwa kiongozi katika vipindi vigumu kisiasa na kiuchumi aliweza kuhakikisha utulivu na kufanya mageuzi makubwa katika nyanja za kisiasa na kiuchumi.

"Mzee wetu pia nie aliesimamia mageuzi ya kisiasa na kufanikiwa kurejesha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, baada ya kufutwa 1965" Alisema rais samia na kuongeza kuwa mchakato huo ndio ulimpatia jina la "Baba wa demokrasia" katika taifa hilo la Afrika mashariki.

Soma pia:Rais wa zamani wa Tanzania afariki dunia

Rais Samia pia amesema Hayati Mwinyi ana mchango endelevu uliozisaidia serikali za awamu zilizofuatia kwani ndiye aliyehamasisha uwekezaji kutoka sekta binafsi na soko huria zilizochangia katika ukusanyaji mapato.

Asifiwa kwa kuiunganisha nchi na ulimwengu

Viongozi mbalimbali wakiwemo mabalozi, viongozi wa jumuiya ikiwemo Afrika mashariki wamehudhuria hafla hiyo,ya kumuaga kiongozi huyo.

kwa upande wake Makamu wa rais wa Nambia Bi Netumbo Nandi-Ndaitwah ambaye alikuwa ni kiongozi pekee wa kigeni aliyezungumza wakati wa kumuaga Mzee Alhasan Mwinyi  katika Uwanja wa Amani mjini Unguja alisema Afrika imempoteza mtu ambaye atakumbukwa kwa mchango wake wa kuliunganisha bara la Afrika.

Unguja, Zanzibara | Gari lililobeba mwili wa rais wa zamani Tanzania Ali Hassan Mwinyi na waombolezaji
Waombolezaji wakiusindikiza mwili wa rais wa zamani wa Tanzani Ali Hassan Mwinyi.Picha: Ericky Boniface/DW

"Mzee Hassan mwinyi alikuwa ni miongoni mwa viongozi wa Afrika ambao walitoa mchango wao makhususi katika kujenga misingi imara wa ushirikiano kati ya watu wa Tanzania na dunia."

Kiongozi huyo ambae alisoma salama za rambirambi za Wanamibia aliongeza kuwa, Mzee Mwinyi ni miongoni mwa "waumini wa ushirikiano" baina ya nchi na nchi na kwamba nchi yake Namibia, imekuwa ni mnufaika wa msingi wa diplomasia alioshiriki kuijenga na ambayo imeendelea kuimarika miongoni mwa mataifa hayo.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, rais wastaafu wa Zanzibar: Dr Amani Karume na Ali Mohamed Shein, Jaji Mkuu wa Tanzania Prof Juma Ibrahim na Abdalla Ali Hassan Mwinyi kwa niaba ya familia, pia walitaja mengi mazuri ya hayati Mzee mwinyi.

Soma pia:Rais wa zamani wa Tanzania afariki dunia akiwa na miaka 98

Baadhi ya wananchi ambao walijitokeza kuaga mwili wa kiongozi huyo walisema watamkumbuka namna ambavyo alifungua nchi, na kukaribisha uwekezaji wa kiuchumi akitumia kauli mbiu yake "Ruksa".

"Nimejifunza mengi sana kupitia kwake kama kiongozi, yaani kiufupi ninayo majonzi makubwa sana," alisema mmoja wa waombolezaji waliojitokeza katika kumuaga kiongozi huyo ambae amekuwa na mchango mkubwa kwa nchi.

"Kitu cha kwanza mimi nachomkumbuka ni wananchi rukhsa ila msiharifu sheria" Miongoni mwa waombolezaji ambao wamekula chumvi aliiambia DW na kuongeza kuwa "badiliko la pili nalokumbuka ni mabadiliko ya kisiasa."

Mwili wa kiongozi huyo ulipelekwa katika msikiti mkubwa wa Jamii Zenjibar na kusaliwa kabla kupelekwa katika Kijiji cha Mangapwani, Kaskazini mwa Mji Mkongwe wa Zanzibar na kuzikwa.

Licha ya kuwa alizaliwa Mkuranga Dar es Salaam, Kijiji cha Mangapwani ndiko alipolelewa na kukuwa hadi kupata mafanikio kadhaa ya uongozi katika maisha yake yote na ndipo alipoanzia chimbuko la mafanikio ya elimu yake.

Buriani Mzee Ali Hassan Mwinyi