1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto 11,000 wauawa ama kukatwa viungo Yemen - UNICEF

12 Desemba 2022

Wakati vita nchini Yemen vikitimia mwaka wake wa nane, Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watoto 11,000 wameshauawa ama kukatwa viungo vyao katika taifa hilo masikini kabisa katika eneo la Ghuba ya Arabuni.

https://p.dw.com/p/4Knyk
Jemen | Unterernährtes Kind
Picha: Mohammed Mohammed/Photoshot/picture alliance

Ripoti iliyotolewa siku ya Jumatatu (Disemba 12) na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) ilisema huenda idadi kamili ya watoto waliouawa na kupoteza viungo vyao inapindukia takwimu rasmi zilizochapishwa, huku maelfu ya wengine wakiwa "kwenye hatari ya kupoteza maisha kutokana na maradhi yanayoepukika ama njaa."

Mkuu wa UNICEF, Catherine Russell, aliwaambia waandishi wa habari kuwa watoto zaidi yamilioni mbilinchini Yemen wana utapiamlo wa kiwango kibaya kabisa, ambapo robo yao ni wale walio chini ya umri wa miaka mitano.

"Wengi wao wanaweza kupatwa na kipindupindu, churuwa na maradhi mengine yanayoweza kukingwa kwa chanjo," alisema mkurugenzi huyo.

Vita nchini Yemen vilizuka mwaka 2014 na kushuhudia kundi la waasi wa Kihouthi likifanikiwa haraka kutwaa udhibiti wa mji mkuu, Sana'a, na mwaka mmoja baadaye muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kuivamia nchi hiyo kwa ajili ya kupambana na waasi hao wanaoshukiwa kuungwa mkono na hasimu mkubwa wa Saudia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Malaki wapoteza maisha

BG Jemen Corona Pandemie medizinische Versorgung
Watoto wakipimwa virusi vya korona nchini Yemen.Picha: Abdulnasser Alseddik/AA/picture alliance

Tangu hapo, malaki ya watu wameshapoteza maisha, ama kutokana na mapigano ya moja kwa moja au kutokana na kunywa maji yasiyo salama, miripuko ya maradhi, njaa ama madhara mengine ya vita. 

UNICEF imethibitisha vifo 3,774 baina ya Machi 2015 na Septemba 2022.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa yalidumu hadi tarehe2 Oktoba, lakini pande hasimu zilishindwa kuongeza muda zaidi baada ya hapo. Tangu kumalizika kwa makubaliano hayo, watoto 62 wameshauawa ama kujeruhiwa, kwa mujibu wa UNICEF.

Russell alitowa wito wa kusainiwa haraka kwamakubalianomengine ya kusitisha mapigano ambayo anasema itakuwa hatua muhimu kuelekea usambazaji wa huduma za kiutu. 

"Ni kutokana na hilo tu ndipo amani endelevu itakapowezesha kuyejenga upya maisha yaliyosambaratiika na kuanza mipango kwa mustakabali wa baadaye. Ili watoto wa Yemen wawe na fursa yoyote ya maisha, lazima wale wenye ushawishi wautumie kuhakikisha wanalindwa na wanasaidiwa." Alisema mkuu huyo wa UNICEF.

Kwa mujibu wa UNICEF, wavulana 3,904 wameshageuzwa kuwa wapiganaji na zaidi ya wasichana wamepewa majukumu ya kivita kama vile kuweka kuwa walinzi kwenye vizuizi vya barabarani. 

Shirika hilo liliomba jumla ya dola milioni 484.4 kukabiliana na hali mbaya ya kibinaadamu inayowaandama watoto wa Yemen.