1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto ndio wahanga wakubwa wa ubakaji

11 Aprili 2013

Watoto ni wahanga wakubwa wa udhalilishaji wa kingono katika maeneo ya mizozo, linalalamika shirika la Uingereza, Save the Children na kuutaja utovu huo kuwa 'maovu makubwa na ya kutisha ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.'

https://p.dw.com/p/18E72
Wahanga wa ubakaji nchini LiberiaPicha: picture-alliance / dpa

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika hilo lisilomilikiwa na serikali, Save The Children, iliyochapishwa jana mjini London, zaidi ya asilimia 70 ya wahanga wa ubakaji katika nchi zilizoathirika zaidi na vita, mfano wa Liberia au Sierra Leone, ni watoto.

Uchunguzi uliofanywa umebainisha kwamba watoto wenye umri wa miaka miwili waliangukia mhanga wa visa vya kinyama vya maprofesa, wakuu wa kidini na wanajeshi waliopelekwa kwa ajili ya kutumikia harakati za kusimamia amani. Uchunguzi huo unazungumzia pia kuhusu vifo vya watoto walioangukia mhanga wa ubakaji au kudhalilishwa kingono na makundi ya wanajeshi.

"Inashtusha kuona idadi ya watoto walioangukia mhanga wa visa vya udhalilishaji wa kingono katika maeneo ya mizozo, ikifikia kiwango cha kutisha kama hicho," amesema Justin Forsyth, ambaye ni mkurugenzi mkuu wa shirika hilo la Save The Children. "Visa vya kuwadhalilisha watoto kingono ni mojawapo ya ushenzi mkubwa na uliofichika wa vita," ameshadidia mkurugenzi huyo.

Logo Save the Children
Nembo ya shirika la Save the Children

Walimwengu wawe macho

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza, William Hague, aliyepania kuwazinduwa watu juu ya athari za ubakaji katika vita, hivi karibuni alikutana na wahanga wa visa hivyo katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, akifuatana na mcheza sinema mashuhuri, Angelina Jolie, ambaye ni mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa anayewashughulikia wakimbizi. Suala hilo limeingizwa pia katika ajenda ya mazungumzo ya mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi nane tajiri kiviwanda ulioanza jana mjini London, Uingereza.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na shirika la Save the Children, baada ya vita nchini Liberia, asilimia 80 ya wahanga wa udhalilishaji wa kingono, kati ya mwaka 2011-2012 walikuwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 17. Wengi wao walibakwa.

Kongo Vergewaltigte Frauen von Luvungi
Wahanga wa ubakaji huko Luvungi katika jamhuri ya kidemokrasi ya KongoPicha: DW/ S. Schlindwein

Madhara ya ubakaji hayana mfano

Shirika la Save the Children kwa mfano limekusanya ushahidi kutoka kwa Pamela wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, aliyebakwa karibu na kambi za wakimbizi. "Ilikuwa siku yangu ya tatu kambini, nilitoka kwenda kuchota maji na watu watatu wakanikamata. Mmoja akanikamata miguu yote miwili na mwengine mikono," amesema Pamela.

Baada ya kunajisiwa alitaka kurejea nyumbani, lakini mamake alikuwa ameshaarifiwa yaliyotokea na alimkatalia ruhusa ya kurerejea nyumbani. Baada ya kufukuzwa na walio wake, Pamela alilazimika kuolewa na yule yule aliyembaka na aliyemkimbia, lakini baadaye akamwacha na mimba ya miezi saba.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters

Mhariri:Josephat Charo