1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto zaidi ya 250,000 huenda wamekufa kutokana na njaa

9 Desemba 2021

Shirika la Save the Children limesema zaidi ya watoto 260,000 walio chini ya miaka mitano Afrika Mashariki, huenda wakawa wamekufa kutokana na njaa au magonjwa yanayohusiana na njaa tangu mwanzoni mwa mwaka 2021.

https://p.dw.com/p/441tb
Tschad Sahel | Hungernot
Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Kwa kutumia data zilizokusanywa na Umoja wa Maraifa, shirika la Save the Children lilitathmini viwango vya vifo kutokana na visa visivyotibiwa vya utapiamlo kwa watoto walio chini ya miaka mitano katika mataifa 8 ya Afrika Mashariki. Kwa makadirio shirika hilo la msaada liligundua kuwa watoto 262,500 huenda wakawa wamekufa kutokana na utapiamlo kati ya mwezi Januari hadi Novemba mwaka huu.

Afrika Mashariki kwa sasa inapitia kipindi kigumu cha athari za mabadiliko ya tabia nchi huku kukiwa na visa vya mara kwa mara vya ukame na mafuriko vinavyosababisha watu wengi kupoteza makazi yao pamoja na ukosefu wa chakula.

soma zaidi: UN: Mamilioni wahitaji msaada wa kiutu Sahel

Wakati jamii Mashariki mwa Kenya, Kusini mwa Somalia na sehemu ya eneo la Ethiopia ikiyumba na kuhangaika kufuatia ukame unaoshuhudiwa katika maeneo hayo sehemu ya Sudan Kusini inabakia kavu bila maji baada ya miaka mitatu ya mvua  isiyotabirika.

Akuol aliye na miaka 16 mama wa mtoto wa miezi 17 Kusini mwa Sudan anahangaika kupata chakula cha kutosha kwake na kwa mwanawe wa kiume. Msaada wa chakula kutoka mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa anaoutegemea umetatizwa kutokana na mvua kubwa.

Akuol anasema anakosa matumaini maana hana chakula cha kumpikia mwanawe na hata nyumba wanamoishi ni sawa na kuishi barabarani, anasema kwa sasa hana wa kumkimbilia.

Vituo vya Afya vinaendelea kuwasajili watiti wanaougua utapiamlo

Äthiopien Hungersnot in Tigray
mmoja ya watoto wanaougua utapiamlo nchini EthiopiaPicha: privat

Kijala Shako, mkurugenzi wa mawasiliano kampeni na vyombo vya habari Mashariki na Kusini mwa Afrika amesema wamesikitishwa na habari kuwa watoto zaidi ya laki mbili Afrika Mashariki huenda wakawa wamekufa kutokana na njaa tangu kuanza kwa mwaka 2021.

Mwaka ambao janga la COVID 19 limeendelea kuathiri maisha ya wengi pamoja na chumi za mataifa mengi pamoja na migogoro inayouwa na kuwakosesha makaazi wengi. Ameongeza kuwa mabadiliko ya tabia nchi yameonyesha makali yake na kuwaathiri watoto kwa kiwango kikubwa

soma zaidi: Janga la virusi vya corona kitisho kwa usalama wa chakula

Vituo vya afya vimeendelea kuwasajili watoto wengi zaidi wanaougua utapiamlo mwaka huu kukiwa na ongezeko la asilimia 16 ndani ya nusu mwaka. Utapiamlo ni aina moja hatari ya hali inayowakumba watoto wasiopata lishe bora. dalili zake ni pamoja na ngozi iliyonyauka, kukonda kupita kiasi kufura kwa vifundo vya miguu pamoja na tumbo kutokana na mishipa ya damu kuvujisha maji chini ya ngozi mwilini.

Kwa sasa asilimia 46 ya watoto walio katika hali hiyo wanapokea matibabu katika sehemu mbali mbali Afrika Mashariki.

Mwandishi: Amina Abubakar /Save the Children

Mhariri: Josephat Charo