Watu 109 wafariki kutokana na mafuriko Rwanda, sita Uganda
3 Mei 2023Televisheni ya taifa ya Rwanda imetangaza leo kuwa juhudi za uokozi kuwatafuta watu waliokwama kwenye nyumba zao zinaendelea.
Gavana wa Jimbo la Magharibi François Habitegeko, amesema kipaumbele chao cha kwanza ni kuzifikia nyumba zote ambazo zimeharibiwa ili kuhakikisha wanawaokoa watu waliokwama.
Habitegeko amesema watu 95 wamekufa katika jimbo hilo. Amesema wilaya zilizoathiriwa zaidi na mvua hizo ni za Rutsiro, Nyabihu, Rubavu na Ngororero.
Wakati huo huo, katika nchi jirani ya Uganda, karibu na mpaka unaopakana na Rwanda, watu sita wamekufa usiku wa kuamkia leo katika wilaya ya Kisoro iliyoko kusini magharibi, baada ya mvua kubwa kunyesha kwenye eneo la milima.
Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Uganda limesema watano waliokifa ni wa familia moja.