Watu 11 wauawa katika mashambulizi Yemen
18 Januari 2022Mauaji hayo yametokea wakati ambapo muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ukirudisha mashambulizi baada ya shambulizi jengine Abu Dhabi ambalo limesababisha hali ya wasiwasi katika eneo la Ghuba.
Duru za kitabibu na walioshuhudia zimeeleza kuwa mashambulizi hayo yalipiga Jumanne kwenye nyumba mbili mjini Sanaa, saa chache baada ya waasi wa Houthi kudai kufanya shambulizi la kombora ambalo liliwaua watu watatu kwenye mji mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu.
Akram al-Ahdal, mmoja wa ndugu wa waliouawa amesema watu 11 wameuawa na bado wanaendelea kuwatafuta walionusurika ambao wamefunikwa kwenye vifusi. Duru za kitabibu pia zimethibisha idadi hiyo ya watu waliouawa.
Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE ambao ni sehemu ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia kupambana na waasi wanaoungwa mkono na Iran, wameapa kujibu vikali shambulizi la Jumatatu, shambulizi la kwanza baya kufanywa ndani ya mipaka yake, ambalo waasi wa Houthi wamedai kuhusika.
Siku ya Jumanne muungano huo ulianzisha mashambulizi mapya yanayozilenga kambi za Houthi na makao yake makuu mjini Sanaa. Hayo yalielezwa na Televisheni ya taifa ya Saudi Arabia, Al-Ekhbariya.
Saudia na Abu Dhabi kushirikiana
Baada ya mashambulizi hayo, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman na mrithi wa kiti cha ufalme wa Abu Dhabi, Mohamed bin Zayed walikubaliana katika mazungumzo yao ya simu kusimama kwa pamoja kukabiliana na vitendo hivyo vya uchokozi.
Marekani imelaani mashambulizi hayo na imeahidi kukabiliana na waasi wa Houthi. Mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani, Jake Sullivan amesema nchi hiyo itashirikiana na Umoja wa Falme za Kiarabu na washirika wake wa kimataifa kuwawajibisha waasi hao.
Nazo Uingereza, Ufaransa na Umoja wa Ulaya pia zikilaani shambulizi hilo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian amesema mashambulizi hayo yanatishia usalama wa Umoja wa Falme za Kiarabu na utulivu wa kikanda.
Mzozo wa tangu 2014
Vita vya Yemen vilianza mwaka 2014 wakati waasi wa Houthi walipouteka mji mkuu, Sanaa na kusababisha mwaka uliofuata vikosi vinavyoongozwa na Saudi Arabia kuingilia kati kuiunga mkono.
Mzozo huo umesababisha janga kwa mamilioni ya wananchi wake ambao wameyakimbia makaazi yao, huku wengi wao wakikaribia kukumbwa na njaa, katika kile ambacho Umoja wa Mataifa umeutaja kuwa mzozo mbaya zaidi wa kibinaadamu duniani.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa hadi mwishoni mwa mwaka 2021, vita vya Yemen vimewaua watu 377,000, kupitia mashambulizi au njaa na magonjwa.
(AFP, DPA)