Watu 118 wauwawa na polisi wa Kenya mwaka 2023
24 Aprili 2024Idadi hiyo ya mauaji ya watu imepungua kwa asilimia 9 kutoka 130 mwaka uliopita, wakati kiwango cha watu wanaopotea chini ya mikono ya vyombo vya dola nacho kikishuka hadi watu 10 katika kipindi hicho. Karibu nusu ya mauaji hayo yalitokea wakati wa operesheni ya kupambana na uhalifu, kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa leo na mashirika kadhaa ikiwemo Human Rights Watch, Amnesty International Kenya na lile la Missing Voices Kenya, yani sauti zilizopotea.
Watu wengine 45 waliuawa wakati wa maandamano yaliyoitishwa na upinzani Kenya kati ya mwezi Machi na Julai mwaka uliopita, kupinga kupanda kwa gharama za maisha. Maandamano hayo dhidi ya serikali ya Rais William Ruto yalishuhudia vurugu za hapa na pale na uporaji, huku upinzani na mashirika ya haki za binadamu yakilishutumu jeshi la polisi kwa matumuzi ya kupita kiasi.
Nikinukuu ripoti hiyo inasema kuwa; "Maafisa wa polisi mara chache hukamatwa kwa kushiriki katika mauaji ya kiholela na kuhusika katika kupotea kwa watu." mwisho wa kunukuu. Tangu kuchaguliwa kwake katika uchaguzi wa 2022, Ruto amesema mara kwa mara kuwa anataka kukomesha vurugu na vitendo vya ukiukaji sheria vinavyotekelezwa na maafisa wa usalama. Polisi nchini Kenya wameshutumiwa na mashirika ya haki za binadamu kwa matumizi ya nguvu ya kupitiliza na kufanya mauaji ya kiholela, haswa katika mitaa ya makaazi duni.
Watu zaidi ya 1000 wanadaiwa kufa mikononi mwa maafisa wa usalama
Aidha pia wamewahi kutuhumiwa kipindi cha nyuma kwa kuendesha vikundi vinavyowalenga wanaharakati na wanasheria wanaochunguza madai ya ukiukwaji wa haki na polisi. Rais Ruto alinukuliwa hivi karibuni akikiri kwamba nchi imewapoteza Wakenya wengi kutokana na mauaji ya kiholela na mauaji yanayohusishwa na siasa. Mnamo mwezi Oktoba 2022, Rais huyo aliahidi kulifanyia mageuzi jeshi la polisi na kutangaza kukivunja kikosi maalumu kinachohofiwa na wengi cha SSU ambacho maafisa wake wametuhumiwa kwa kuwapoteza watu na mauaji.
Kwa mujibu wa shirika la Missing Voices, watu 1,350 wamekufa mikononi mwa maafisa wa usalama tangu shirika hilo lilipoanza kukusanya taarifa mwaka 2007. Kumekuwa na hatua kidogo za kisheria dhidi ya polisi wanaofanya mauaji hayo. Februari mwaka jana hata hivyo, askari polisi watatu walihukumiwa vifungo vya kuanzia miaka 24 jela hadi adhabu ya kifo kwa mauaji ya mwaka 2016 ya watu watatu akiwemo wakili.