Watu 14 wauwawa katika uvamizi wa mifugo Samburu
8 Novemba 2021Afisa Mkuu wa Polisi eneo hilo Alex Rotich amethibitisha kutokea kwa kisa hicho huku akisema kuwa usalama umeimarishwa.
Waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali ya jimbo la Samburu huku walioaga dunia wakipelekwa katika makafani ya hospitali hiyo. Wakati huo huo, ulinzi umeimarishwa katika eneo hilo kwa sasa baada ya maafisa wa usalama kupelekwa huko. Hata hivyo wakazi wanaendelea kuishi kwa hali ya wasiwasi kwani sio mara ya kwanza kwa uvamizi kushuhudiwa.
Soma Taharuki yatanda mpaka wa Isiolo na Samburu
Polisi wamewapata Mifugo 1,000 waliokuwa wameibiwa kwa mujibu wa Afisa Mkuu wa Polisi wa Samburu Alex Rotich. "Miili ambayo tumepata kuona hapa ni tisa ya wavamizi, na miili tano kutoka kwa jamii iliyvamiwa, kwa ujumla ni miili 14 ambayo iko kwa kichaka.”
Alex amewataka wakazi kutulia akisema kuwa serikali inafanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa inawalinda pamoja na mali yao. Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya serikali, yamelaani kuongezeka kwa visa vya ukosefu wa usalama katika maeneo mbali mbali ya taifa, huku likisema kuwa zaidi ya watu 20 wamewaua katika majimbo ya Samburu na Marsabit. Jumatano, watu 14, waliuawa, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa baada ya wavamizi kutoka Turkana kushambulia eneo la Samburu Kaskazini watu sita wakiripotiwa kufariki na idadi ya mifugo wasiojulikana kuibiwa.
Mwakilishi wa Wanawake wa jimbo la Samburu Maison Leshoomo ni miongoni mwa wale waliofika katika kijiji cha Suyan kuomboleza na familia zilizoathiriwa. Ameikosoa idara ya usalama kwa kuzembea kufika kwa wakati uliofaa kukabiliana na wavamizi hao.
"Ikiwa mtu mmoja atakufaa mahali, utaona ndege wa polisi wanavyofika kwa haraka. Hatujaona chochote ama watu kutoka Nairobi kuja kuona watu wanazozania nini?” alisema Maison Leshoomo
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya serikali Stephen Cheboi amesema hawatakubali mauaji ya raia wasio na kuitaka serikali kukaza mkanda. Aidha amesema hali ya wasiwasi inayoshuhudiwa nchini kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu inatia wasiwasi.
Cheboi amewataka viongozi katika maeneo yaliyoathirika kushirikiana kutafuta suluhisho ya kudumu kuhusu mizozo hiyo ambayo hutokea kila mara. Hali ya ukosefu wa usalama, inazidishwa kuwa mbaya na ukame ambao unayakabili maeneo ya kaskazini mwa Kenya.
Shisia Wasilwa, DW, Nairobi