1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 15 wafariki kwenye ajali ya barabarani Kenya

Wakio Mbogho9 Januari 2024

Ajali hiyo inaendeleza msururu wa ajali zinazoshuhudiwa nchini humo licha ya ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO, kuonesha kwamba ajali zimepunguwa ulimwenguni.

https://p.dw.com/p/4b1nE
Watu 15 wafariki na wengine 9 kujeruhiwa kwenye ajali ya barabara ya Nakuru kuelekea Eldoret
Watu 15 wafariki na wengine 9 kujeruhiwa kwenye ajali ya barabara ya Nakuru kuelekea EldoretPicha: AFPTV/AFP/Getty Images

Kulingana na ripoti za polisi, basi lililokuwa linasafiri kutoka taifa la Kongo kuelekea Nairobi liligongana ana kwa ana na matatu iliyokuwa inatoka Nairobi kuelekea Eldoret katika eneo la Twins Bridge, Mau Summit Kaunti ya Nakuru, asubuhi ya leo. Abiria wote waliokuwa kwenye matatu waliaga dunia. Juda Gathenge, kamanda wa polisi eneo hilo amesema dereva wa basi alitoweka baada ya ajali.

"Basi lilikuwa linashuka kwenye mlima na matatu ilikuwa inapanda. Dereva wa basi alipoteza mwelekeo na wakagongana ana kwa ana. Tumewapoteza watu 15 kwenye ajali hiyo. Kati yao wakiwemo watoto saba.”

Msururu wa ajali Nakuru

Watu saba waliojeruhiwa wanapata matibabu hospitalini, wengine 38 waliopata majeraha madogo wameweza kupata huduma ya kwanza kutoka kwa wahudumu wa shirika la msalaba mwekundu.

Ajali hii inajiri siku tano baada ya watu wengine watano kupoteza maisha kwenye barabara hiyo kuu ya Nakuru-Eldoret. Wiki moja iliyopita ajali nyingine kati ya trela na matatu iliyofanyika kwenye barabara hiyo eneo la Nakuru ilisababisha vifo vya watu saba.

Racheal Maru, mhudumu katika shirika la msalaba mwekundu nchini anapendekeza upanuzi wa barabara kuu kutoka Nairobi hadi Eldoret ukamilishwe ili kuzuia ajali hizi.

Maafa ya barabarani yapungua kwa silimia tano

Idadi ya vifo kutokana na ajali za barabani inapungua kwa silimia tano ulimwenguni
Idadi ya vifo kutokana na ajali za barabani inapungua kwa silimia tano ulimwenguniPicha: imago images/Xinhua

Kulingana na ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni ya Disemba mwaka uliopita, vifo kutokana ajali za barabarani kote ulimwenguni vimepungua kwa kiasi cha asilimia tano tangu mwaka 2010.

Lakini nchini Kenya hali ni tofauti kwani idadi ya ajali barabarani inaongezeka, ikiripotiwa kwamba zaidi ya watu elfu nne walipoteza maisha barabarani mwaka 2023.

Tawkimu za mamlaka ya Kenya ya usafiri na usalama barabarani, NTSA, Kenya zinaonesha kwamba mwaka 2022 vifo 4,690 vilirekodiwa kutokana na ajali barabarani ikilinganishwa na vifo 4,579 vilivyorekodiwa mwaka 2021. Imebainika kwamba sababu kuu ya ajali hizi ni uendeshaji mbaya wa magari, matumizi ya vileo na dawa za kulevya kwa madereva.