1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 16 wauawa katika shambulizi la Kabul

18 Januari 2014

Watu 16 wameuawa wakiwemo wafanyakazi wanne wa Umoja wa Mataifa na raia wengine wa kigeni, katika mlipuko wa bomu na shambulizi la risasi lililofanywa kwenye hoteli moja ya mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

https://p.dw.com/p/1At1V
Afghanistan Kabul Explosion 17.01.2014
Picha: Johannes Eisele/AFP/Getty Images

Mlipuaji wa kujitoa mhanga amejilipua nje ya mgahawa mmoja mjini Kabul uliokuwa umejaa raia wa kigeni na wa Afghan wa tabaka la juu, wakati watu wengine wawili waliokuwa na bunduki waliingia ndani ya hoteli hiyo kupitia mlango wa nyuma na kuanza kufyatua risasi kiholela jana usiku.

Taliban imedai mara moja kuhusika na shambulizi hilo lililofanywa katika hoteli ya La Taverna du Liban, ikiwa ni sehemu ya ongezeko la harakati zake za mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni na serikali ili kutuma ujumbe kuwa wanamgambo hao hawaendi kokote wakati jeshi la kimataifa linaloongozwa na Marekani linapokaribia kumaliza operesheni zake za kivita nchini humo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Mkuu wa polisi mjini Kabul, Jenerali Mohammad Zahir Zahir amesema watu 16 waliouawa wote walikuwa ndani ya mgahawa huo. Amesema raia wa kigeni na wa Afghan ni miongoni mwa waliouawa, lakini hakutoa maelezo zaidi. Maafisa wamesema watu wengine wanne walijeruhiwa.

Suicide bombing in Kabul's diplomatic quarter

Ban alaani shambulio hilo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amethibitisha kuwa wafanyakazi wanne wa Umoja wa Mataifa ni miongoni mwa waliouawa, ijapokuwa bado hawajatambuliwa. Ban amelaani vikali shambulizi hilo akisema mashambulizi ya aina hiyo yanayowalenga raia hayawezi kamwe kukubalika na yanakiuka sheria za kimataifa.

Mwakilishi wa Shirika la Fedha Ulimwenguni – IMF nchini Afghanistan Wabel Abdallah, pia alikuwa miongoni mwa waliouawa, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkuu wa IMF Christine Lagarde.

Mwakilishi huyo mwenye umri wa miaka 60 kutoka Lebanon, aliteuliwa katika wadhifa huo mwaka wa 2008. Ofisi ya mambo ya nje ya Uingereza imethibitisha kuwa raia wake mmoja ni miongoni mwa waliouawa, huku Canada pia ikisema raia wake waliwili wamekufa katika shambulizi hilo.

Mjini Washington, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Jen Psaki amesema Marekani imelaani vikali tukio hilo la kigaidi. Mgahawa huo, hutumiwa sana na wanadiplomasia wa kigeni, wafanyakazi wa misaada, waandishi wa habari na wafanyabiashara. Msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid amedai kuwa shambulizi hilo liliwalenga maafisa wa ngazi ya juu wa Ujerumani. Mjini Berlin, Wizara ya Mambo ya Kigeni imesema inaitathimini ripoti hiyo.

Mwandishi. Bruce Amani/AP

Mhariri: Ssessanga Iddi