1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 30 wauawa uchaguzi wa Pakistan

25 Julai 2018

Watu 30 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa kwenye kituo kimoja cha kupigia kura hivi leo katika jimbo la Baluchistan katika siku ambayo mamilioni ya Wapakistan wameshuka vituoni kwa ajili ya uchaguzi mkuu.

https://p.dw.com/p/323Ei
Pakistan Quetta Anschlag bei Parlamentswahl
Picha: Reuters/N. Ahmed

Kwa mujibu wa afisa mmoja kwenye mji wa Quetta ulio kusini magharibi mwa Pakistan, Hashim Ghilzai, mshambuliaji aliyejifunga mabomu alikuwa akijaribu kujipenyeza kwenye kituo cha kupigia kura, ndipo alipojiripua na kuwauwa watu wapatao 30 pamoja naye mwenyewe. 

Daktari Muhammad Jaffar wa Hospitali ya Sandeman walikopelekwa baadhi ya maiti na majeruhi aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba miongoni mwa waliouawa ni watoto wa miaka minane na sita.

"Hadi sasa tumepokea hapa miili 21, akiwemo msichana wa miaka minane na mvulana wa miaka sita", alisema daktari huyo.

Kupitia shirika lake rasmi la habari, Amaq, kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS) lilidai kuhusika na mashambulizi haya, yakiwa mashambulizi ya karibuni kabisa kwenye jimbo masikini kabisa la Baluchistan, ambalo limekuwa kiini cha makundi kadhaa ya uasi na ya sias kali.

Jimbo hili lilikumbwa na mkururo wa mashambulizi yaliyouwa zaidi ya watu 180 kote nchini Pakistan wakati wa kampeni za uchaguzi huu wa leo, yakiwemo yale ya wilayani Mastung ambayo yaliangamiza maisha ya watu 153, akiwemo mwanasiasa mashuhuri wa huko, Siraj Raisani.

Siraji alikuwa mmoja wa wagombea watatu waliouawa na wanamgambo wa IS kwenye kampeni hizo.

Mashambulizi yazidi licha ulinzi kuimarishwa

Pakistan Quetta Anschlag bei Parlamentswahl
Maafisa usalama wakikusanyika kwenye kituo cha kura mjini Quetta, kusini magharibi mwa Pakistan, ambako mshambuliaji wa kujitoa muhanga aliwauwa watu 30 siku ya Jumatano (25 Julai 2018).Picha: Getty Images/AFP/B. Khan

Mashambulizi ya hapo jana kwenye jimbo hilo hilo yalimuua polisi mmoja na kuwajeruhi wengine watatu, baada ya bomu kurushwa katika kituo kimoja ya kura kwenye kijiji cha Koshk, wilayani Khuzdar.

Serikali imesambaza wanajeshi 370,000 na askari polisi 450,000 nchi nzima kusimamia ulinzi kwenye uchaguzi huu wa leo.

Kutokana na sababu za kiusalama, tume ya uchaguzi imetangaza kusitisha huduma za simu na intaneti kwenye baadhi ya wilaya za Baluchistan. 

Upigaji kura kwenye baadhi ya vituo katika mji mkuu wa Pakistan, Islamabad, na pia kwenye mji mkuu wa jimbo la Punjab uliripotiwa kwenda taratibu, huku polisi wakiwakamata watu wenye kura zilizokwishapigwa. 

Kwa mujibu wa uchunguzi wa mwisho wa maoni, si yeyote kati ya nyota wa kriketi aliyegeuka mwanasiasa, Imran Khan, na waziri mkuu wa zamani aliyehukumiwa kifungo cha miaka kumi jela kwa ufisadi, Nawaz Sharif, anayeweza kupata ushindi wa moja kwa moja. 

Licha ya Khan kuonekana kuongoza kidogo kwenye matokeo ya jumla ya uchunguzi huo wa maoni, kwenye maeneo ambayo Sharif ana wafuasi wengi, kama ilivyo Punjab, uungaji mkono wa Khan ni wa chini mno kuweza kumpa ushindi wa wazi kitaifa. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP/AP
Mhariri: Saumu Yussuf