Watu 35 wauawa kwenye kituo cha treni mashariki mwa Ukraine
8 Aprili 2022Mamlaka mashariki mwa Ukraine zimesema watu 35 wameuawa na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa kufuatia mashambulizi ya kombora kwenye kituo cha treni katika mji wa Kramatorsk siku ya Ijumaa (8 Aprili) wakati raia wakikimbilia kulihama eneo la Donbas linalokabiliwa na operesheni kubwa ya kijeshi ya Urusi.
Waandishi wa habari wa shirika la AFP wmeripoti kuona miili ya watu 20 ikiwa imekusanywa na kuwekwa mifuko ya plastiki karibu na kituo hicho cha treni.
Waandishi hao wanasema damu imeenea huku mabegi yakichawanyika huku na kule nje ya jengo la kituo hicho.
Mabaki ya roketi kubwa lenye maandishi "kwa watoto wetu" kwa Kirusi lilionekana karibu na jengo hilo.
Watu wapatao 4,000, wengi wao wanawake, watu wazima na watoto, walikuwepo kwenye kituo hicho cha treni wakati mashambulizi hayo yanafanyika kwa mujibu wa Meya wa Kramatorsk, Oleksander Honcharenko.
Hata hivyo, Wizara ya Ulinzi ya Urusi imekanusha kwamba vikosi vyake vimehusika na mashambulizi dhidi ya kituo hicho cha treni, akisema kuwa aina ya kombora lililotumika linatumiwa tu na jeshi la Ukraine, ambalo ni sawa na lile lililouwa watu 17 katikati mwa mji wa Donetsk mnamo tarehe 14 Machi.
Mawaziri wa ulinzi wa Uturuki, Uingereza na Italia wakutana
Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, Ben Wallace, na mwenzake wa Italia, Lorenzo Guerini, walitarajiwa kuitembelea Istanbul siku ya Ijumaa kwa mualiko wa mwenzao, Hulusi Akar.
"Kwenye mkutano huo, majadiliano yatajikita kwenye mahusiano ya ulinzi na usalama kati ya nchi hizi na masuala ya kikanda na maendeleo ya hali nchini Ukraine." Ilisema taarifa iliyotolewa na pande hizo tatu.
Uturuki, ambayo ni mwanachama wa NATO, ina mpaka wa baharini na Ukraine na Urusi kwenye Bahari Nyeusi na ina mahusiano mazuri na pande zote mbili, hali iliyoifanya kubeba jukumu la upatanishi kwenye mgogoro wa sasa.
Hadi sasa imefanikiwa kuwakutanisha mawaziri wa mambo ya kigeni wa Urusi na Ukraine pamoja na wapatanishi na sasa inapanga kuwakutanisha maraisi wa pande hizo mbili.
Japan yawafukuza wanadiplomasia wa Urusi
Hayo yakijiri, Japan ilisema siku ya Ijumaa kwmaba ingeliwafukuza maafisa wanane wa kibalozi wa Urusi ikisema vitendo vya Moscow nchini Ukraine havikubaliki na ni uvunjaji wa sheria za kimataifa.
"Kutokana na uamuzi wa kina wa nchi yetu, tumeomba kufukuzwa kwa wanadiplomasia kutoka Ubalozi wa Urusi nchini Japan na maafisa kutoka Ofisi ya Biashara ya Shirikisho la Urusi." Ilisema taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Japan.
Hatua hii inafuatia wimbi la hatua kama hizo barani Ulaya, wakati washirika wa Kimagharibi wakiituhumu Urusi kwa uhalifu wa kivita uliotendwa na wanajeshi wake karibu na mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.
Ujerumani yataka Putin ashitakiwe kwa uhalifu wa kivita
Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani ametowa wito wa kuundwa kwa mahamakama maalum ya uhalifu wa kivita dhidi ya Rais Vladimir Putin wa Urusi na waziri wake wa mambo ya kigeni, Sergei Lavrov.
Kwenye mahojiano yaliyochapishwa siku ya Ijumaa (Aprili 8) na gazeti la Der Spiegel, Rais Steinmeier alisema: "Mtu yeyote mwenye kuhusika na uhalifu huu atapaswa kujieleza, wakiwemo wanajeshi, makamanda na wale wenye dhamana za kisiasa."
Kauli hiyo nzito kutolewa na kiongozi wa juu wa nchi huenda ikachochea zaidi mpasuko uliopo kati ya Ujerumani na Urusi, huku Ujerumani ikitegemea kiwango kikubwa cha nishati yake kutoka Urusi.