1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 45 walikufa wakati wa kumuaga Marehemu Magufuli

30 Machi 2021

Polisi ya Tanzania imesema watu 45 walifariki kufuatia mkanyagano ulioshuhudiwa Marchi 21 jijini Daresalaam katika tukio la waombolezaji kutoa heshima ya mwisho kwa John Pombe Magufuli.

https://p.dw.com/p/3rMwY
Tansania Trauer um Ex-Präsident John Joseph Pombe Magufuli
Picha: Mwanza Dotto Bulendu/DW

Kamanda wa kanda ya jiji hilo la Daresalam Lazaro Mambosasa ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kulikuwa na umati mkubwa wa watu waliotaka kuingia katika uwanja wa michezo wa Uhuru na baadhi yao walikosa subira na kujaribu kuingia kwa mabavu katika uwanja huo na hatimae kusababisha hali ya mkanyagao.

Watu watano walikuwa wa familia moja kati ya watu 45 waliokufa katika ajali hiyo.

soma zaidi: Hayati Magufuli aagwa nyumbani kwake Chato

Kisa cha mwanamke mmoja na watoto wanne kufariki katika ajali hiyo ndicho kilichoripotiwa awali na idadi kamili ya waliokufa kwenye tukio hilo haikuwahi kutangazwa wakati huo.

Kadhalika kamanda huyo wa jeshi la polisi amesema watu wengine wengi walijeruhiwa lakini wengi waliruhusiwa kuondoka hospitali.

Aliyekuwa rais wa Tanzania Dk John Joseph Pombe Magufuli alifariki dunia tarehe 17 mwezi Machi kutokana na matatizo ya Moyo na alizikwa tarehe 26mwezi huo nyumbani kwako Chato mkoani Geita.