Watu 6 wauawa katika maandamano ya upinzani Kenya
12 Julai 2023Kwa upande wake, polisi wameyapiga marufuku maandamano ya leo na waliopatikana barabarani walikamatwa. Upinzani unapinga sheria mpya ya fedha inayowabinya Wakenya kwa nyongeza ya kodi zinazonuwia kuiongezea serikali pato. Tayari, kesi kamili inasubiriwa kuanza baada ya Mahakama Kuu kuamuru kuwa utekelezaji wa sheria hiyo usitishwe kwa muda.
Soma pia: Mtu mmoja ameuwawa katika maandamano Kenya
Watu sita wameuawa kwenye maandamano katika kaunti za Machakos na Kajiado. Watatu walipigwa risasi hadi kufa mjini Kitengela na mwengine aliuawa Emali. Wengine wawili walipoteza maisha yao mtaani Mlolongo. Akizungumza akiwa jijini Nairobi, kinara wa ODM iliyo chama msingi cha muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga alishikilia kuwa wataishinikiza serikali hadi pale Rais William Ruto hadi pale kilio cha wananchi kitakaposikika. Raila Odinga aliwashukuru wakenya waliojitokeza kuandamana hata baada ya polisi kuwanyima vibali vya kukutana:
Hapa Nairobi, kiongozi wa Azimio Raila Odinga alilazimika kufutilia mbali mhadhara uliopangwa kufanyika kwenye uwanja wa Kamukunji hii leo. Uamuzi huo ulifikiwa baada ya wao kupokea taarifa kuwa maafisa wa polisi walipanga kuwavamia wafuasi wao kwa risasi. Kwa upande wake, Inspekta Mkuu wa Polisi Japheth Koome alisisitiza kuwa maandamano ya leo ni haramu kwani hawakutoa vibali. Waliokuwa na ujasiri na kufika barabarani walijikuta katika hali ya mshikemshike walipohangaishwa na polisi
Soma pia: Polisi Kenya yatumia nguvu kuziwua maandamano dhidi ya kodi
Katika eneo la Mlolongo, waandamanaji walilivuruga eneo la barabara kuu na kuung'oa uzio maalum kabla ya polisi kuingilia kati. Huko Meru, kiongozi wa chama cha NARC Kenya Martha Karua ambaye ni mmoja wa viongozi wa Azimio alilazimika kutumia pikipiki baada ya polisi kuwazuia kuingia kwenye hoteli moja mjini humo.
Martha Karua na waziri wa kilimo wa zamani Peter Munya walishuka kwenye magari yao na kupanda pikipiki kuelekea sehemu nyengine. Peter Munya ni mwandani wa kinara wa ODM Raila Odinga ila hajakuwa akionekana kwenye maandamano ya kuishinikiza serikali ya Kenya Kwanza.
Katika eneo la mpakani la Busia, kiongozi wa chama cha Roots, George Wajackoya aliyeandamana na mwakilishi wa wanawake, Catherine Omanyo, walishindwa kuongoza maandamano baada ya vijana waliojawa na ghadhabu kuurushia msafara wao mawe.
Kulingana na vijana hao, maandamano ni hujuma kwa uchumi kwani serikali kuu na ile ya kaunti zinajitahidi kuufufua uchumi.
Huko ukanda wa pwani, viongozi wa Azimio walilazimika kuwarai maafisa wa polisi kuwaachia huru wafuasi wao waliojitokeza kuandamana na kukamatwa. ZamZam Mohamed ni mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Mombasa.
Kwa upande mwengine, viongozi wanaoegemea upande wa Kenya Kwanza wametoa wito wa kinara wa upinzani Raila Odinga kukamatwa kwa kuongoza maandamano kote nchini. Wakiongozwa na mbunge wa Kimilili Didmus Baraza, wabunge wa Kenya Kwanza wanawataka wafuasi wao kumkamata Raila iwapo polisi hawatafanya hivyo katika kipindi cha saa 24.
Vurumai hizo zimetokea wakati Rais William Ruto anampokea rais wa Iran Ebrahim Raisi aliye ziarani barani Afrika kwa mara ya kwanza.