1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 70 wafariki Pakistan kufuatia moto kwenye treni

Oumilkheir Hamidou
31 Oktoba 2019

Watu wasiopungua 70 wameuwawa na dazeni kadhaa kujeruhiwa baada ya jiko la gesi kuripuka ndani ya treni iliyokuwa ikiwasafirisha waumini waliokuwa njiani kwenda kufanya ziara ya kidini nchini Pakistan.

https://p.dw.com/p/3SFr7
Pakistan Zugunglück - Feuer in einem Passagierzug
Picha: Reuters/Jawedasrar Siddiqui

Picha za televisheni zinaonyesha moto unaofuka ndani ya mabehewa matatu ya treni huku vilio vikihanikiza ndani ya treni hiyo katika eneo la vijijini la mkoa wa kati wa Punjab.

Baadhi ya abiria-wengi wao wakiwa waumini waliokuwa njiani kwenda katika ziara ya kidini katika mji wa mashariki wa Lahore, walikuwa wakipika chakula cha asubuhi pale majiko yao mawili ya gesi yaliporipuka-Ali Nawaz, afisa wa ngazi ya juu wa shirika la safari za reli la Pakistan ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP.

Wapakistan wengi wanabeba vyakula wanapokuwa katika safari ndefu lakini majiko ya gesi yamepigwa marufuku. Ali Nawaz anasema uchunguzi unafanywa kuhusu ajali hiyo.

Televisaheni za Pakistan zimeonyesha jinsi dazeni za watu walivyokusanyika njiani kuangalia jinsi moto unavyofuka ndani ya mabehewa  ambayo yaliachana na sehemu nyengine ya treni.

Waziri Mkuu Imran Khan ameamuru uchunguzi juu yakisa hicho kufanywa mara  moja

China Peking Imran Khan trifft Xi Jinping
Waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan Picha: Reuters/P. Song

Vikosi vya  zimamoto vimefika haraka katika eneo hilo karibu na wilaya ya Rahim Yar Khan. Watumishi wa mashirika ya uokozi na wanajeshi pia wameonekana wakisaidia. Miili ya wahanga wa ajali hiyo iliyofunikwa shuka nyeupe imekuwa ikiondolewa.

"Kwa mujibu wa habari zilizotufikia kutoka eneo la ajali, zaidi ya watu 70 wameuwawa na 40 kujeruhiwa", waziri wa afya wa mkoa huo Yasmin Rashid ameliambia shirika la habari la AFP.

Majeruhi wamepelekwa katika hospitali ya mji wa karibu na hapo wa Rawalpindi na miji mengine ya wilaya ya Rahim Yar Khan ameongeza kusema waziri Yasmin Rashid na kuongeza "maiti 18 tu ndizo zilizoweza kujulikkana ni za nani."

Waziri mkuu Imran Khan ameelezea masikitiko yake kwa yaliyotokea na kuwapa mkono wa tanzia familia za wahanga pamoja na kuwaombea wapone haraka majeruhi. Waziri mkuu Imran Khan anasema ameamuru uchunguzi wa kina ufanywe kuhusu kilichotokea.

Vyomvo vya habari vinasema baadhi ya abiria wameuwawa walipokuwa wakijaribu kuchupa huku treni hiyo ikiendelea kwenda.

Ajali za treni huripotiwa mara kwa mara nchini Pakistan. Julai iliyopita watu 23 waliuwawa katika wilaya hiyo hiyo pale treni iliyokuwa ikitokea mjin wa mashariki wa Lahore ilipogongana na treni ya mizigo.

Chanzo AFP