Watu 73 wafariki katika ajali ya treni DRC
14 Machi 2022
Treni ya mizigo iliyokuwa ikisafiri kutoka Luena kwenda mji wa madini wa Tenke iliacha njia katika eneo baina ya kijiji cha Kitenta na cha Buyofwe, katika wilaya ya Lubudi. Idadi iliyokuwa imetolewa awali ilikuwa sitini, ila miili mingine iligunduliwa.
Ujumbe wa serikali ya mkoa wa Lualaba ukiongozwa na waziri wa mambo ya ndani na usalama wa mkoa huo, Déodat Kapenda, ulilizuru eneo hilo la ajali. Halafu Waziri Kapenda alitoa taarifa rasmi ya ajali ifuatavyo.
''Watu sabini na tatu wamekufa, majeruhi 125 wakiwemo 28 wenye majeraha makubwa. Tulishuhudia ajali hiyo mbaya na kwa wale ambao bado wako hai, mipango imefanywa ili kupewa huduma bora.''
Soma pia: Viongozi wa kidini Congo waunga mkono amani
Baadhi ya mashahidi wamesema kwamba ajali hiyo ilitokana na kukatika ghafla kwa chuma kinachounganisha mabehewa na kusababisha treni na mabehewa kudondokea kwenye korongo.
Ukosefu wa vyombo vingine vya usafiri katika eneo hilo unawasukuma kila mara wakaazi kuvamia treni za mizigo, na hilo ni tatizo kubwa kama alivyosema Fabien Mutomb, mkurugenzi wa Kampuni ya Kitaifa ya Reli ya Kongo (SNCC),
''Hili ni tatizo linalotuathiri sana kama taifa. Tuna treni za abiria, lakini wenzetu wanapendelea kupanda treni za mizigo. Hili ni tatizo na tutajitahidi kufanya kila liwezekanalo ili pamoja na mkoa wa Lualaba tuepuke matatizo ya aina hiyo.''
Njia za reli pamoja na treni nyingi hapa Kongo ni za tangu ya enzi ya ukoloni na hivyo zimeshachakaa. Jambo linalosababisha ajali kutokea mara kwa mara nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.