1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu bilioni 2.5 hawana vyoo salama duniani

19 Novemba 2013

Tarehe 19 mwezi Novemba kila mwaka ni siku ya choo duniani. Kiasi ya watu bilioni 2.5 duniani hawana vyoo salama na vya kisasa na wengine bilioni moja hawana choo kabisa

https://p.dw.com/p/1AKZO
Picha: UNHCR/S.Schulman

Kulingana na umoja wa Mataifa ,kila mwaka zaidi ya watoto 800,000 walio chini ya umri wa miaka mitano hufa kutokana na kuharisha, chanzo kikuu kikiwa ni ukosefu wa usafi.

Ukosefu wa vyoo visafi mashuleni pia unawazuia watoto wengi hasa wa kike kushindwa kusoma vizuri hasa baada ya kuvunja ungo. Shule zilizo na vyoo vizuri vinachangia asilimia 11 ya wasichana kuhudhuria masomo.

Wanawake pia walio na hakikisho la kuwa na faragha na usalama wanapokwenda haja,hawako katika hatari ya kushambuliwa na kubakwa ikilinganishwa na wasio na vyoo.

Siku ya choo duniani inatambuliwa na Umoja wa Mataifa

Umoja wa Mataifa umekuwa ukijulikana kuadhimisha mafanikio katika nyanja kama za kisiasa,haki za binadamu,kuwapa uwezo makundi ya watu mbali mbali na hata afya kama siku ya ukimwi duniani,siku ya saratani,siku ya uhuru wa vyombo vya habari,siku ya maji duniani,siku ya wakimbizi na siku nyinginezo,lakini kutambua na kuadhimisha umuhimu wa kuwa na choo na viwe salama hilo halijkuwa limezingatiwa licha ya kuwa kuenda haja ni sehemu muhimu ya maisha ya mwanadamu.

Waliohudhuria siku ya choo duniani mjini Berlin
Waliohudhuria siku ya choo duniani mjini BerlinPicha: AP

Ndiposa mwaka jana mwezi Julai,baraza kuu la umoja wa Mataifa lililoshirikisha nchi wanachama 193 lilipitisha azimio lililowasilishwa na Singapore linaloitambua siku hii ya leo kuwa siku ya choo duniani.Hii ikiwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 68 katika historia ya umoja huo kwa suala la kutumia choo kutambulika na kupewa uzito unaostahili.

Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Ban ki Moon akizindua kampeini ya kukomesha kwenda haja kubwa maeneo yaliyo wazi ifikapo mwaka 2025, amesema usafi hasa katika maeneo ya kwenda haja ni muhimu kwa afya na mazingira ya mwanadamu.

Ban amesema lazima itikadi za kale zivunjwe kuhusu kutozingatia usafi na matumizi ya vyoo ili kuwe na maendeleo na kuongeza kwa kufanya kazi kwa pamoja na kuwa na mijadala wazi kuhusu umuhimu wa vyoo na usafi, basi afya ya robo ya idadi ya watu duniani itaboreka.

Simu wanazo ila vyoo hawana

Kulingana na tume ya uchumi ya Umoja wa Mataifa barani Ulaya UNECE,watu watu bilioni sita kati ya watu bilioni saba duniani kwa sasa wanamiliki simu za mkononi ilhali ni watu bilioni 4.5 tu walio na choo.

Mwanamke nchini Ethopia akionyesha choo chake kilipo
Mwanamke nchini Ethopia akionyesha choo chake kilipoPicha: Richard Hanson

Licha changamoto zilizoko,hatua kubwa zimepigwa.Tangu mwaka 1990,watu bilioni 1.8 duniani wamepata huduma ya kuwa na mazingira safi kupitia kuondoa maji taka na kuchimbwa kwa vyoo na idadi ya watu wanaokwenda haja kubwa maeneo yaliyo wazi imepungua kwa watu milioni 272 duniani.

Hata hivyo himizo linatolewa kuhakikisha ujumbe wa umuhimu wa kuwa na vyoo,kujua kuvitumia vizuri na kuwa na vyoo katika maeneo salama unawafikia watu bilioni 2.5 kote duniani ambao bado wanakosa huduma hii muhimu inayopunguza magonjwa kama kipindu pindu,kuendesha na magonjwa mengine ya kuambukizana kutokana na uchafu na mbali na hivyo matumizi ya choo yanaleta faragha na stara kwani ukosefu wa choo ni jambo la kudhalilisha.

Mwandishi: Caro Robi/ap/Ips

Mhariri: Yusuf Saumu