Watu kadhaa wafa kutokana na joto kali Marekani na Canada
30 Juni 2021Watu hao mia moja walikufa kwenye jimbo la Canada la British Columbia na kwenye mji wa Burnaby mashariki ya Vancouver. Polisi nchini Canada wamesema watu zaidi ya 25 walikufa katika muda wa saa 24. Polisi wamewataka watu kuwa macho ili kuwaangalia majirani zao waliomo katika hatari kubwa na hasa wazee.
Mkuu wa idara ya uchunguzi wa vifo kwenye jimbo la British Columbia amesema idara yake imeorodhesha idadi kubwa ya vifo kwenye maeneo yaliyokumbwa na joto kali nchini Canada. Idara hiyo imeorodhesha vifo 223 kati ya Ijumaa na Jumatatu.Vituo kadhaa vya kupoza joto vimefunguliwa kwa ajili ya kuwasaidia watu kwenye jimbo la Vancouver. Kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa joto kali linatarajiwa kuendelea kuzikumba sehemu kadhaa nchini Canada.
Nchini Marekani pia joto limefikia viwango ambavyo havijawahi kushuhudiwa katika miji ya kaskazini magharibi ya Portland na Seattle tangu kuanza kwa utaratibu wa kuorodhesha vipimo vya joto mnamo mwaka 1940. Miji katika jimbo la Oregon pia imekumbwa na joto kali kupita kiasi. Kwenye maeneo ya mashambani wakulima wameweza kuona jinsi mashamba na mifugo ilivyoathirika. Mfanyakazi kutoka idara ya jamii Verna Fisher ameeleza kuwa watu wengi watahitaji kupelekwa hospitali na wengi watakuwa wagonjwa sana kutokana na hali hii ya joto kali kwa sababu hawafahamu namna ya kujihudumia wao wenyewe.
Kwa mujibu wa taarifa ya idara ya taifa ya utabiri wa hali ya hewa, mji wa Portland ulifikia kipimo cha nyuzi joto 46 wakati mji wa Seattle ulifikia nyuzi joto zaidi ya 42. Wataalamu wanasema mabadilikio ya tabia nchi yanatarajiwa kuongeza mawimbi ya joto kali ya mara kwa mara.
Mawimbi hayo ya joto kali nchini Canada na Marekani yamesababishwa na shinikizo la hewa ya moto kuanzia kwenye jimbo la California hadi maeneo ya nchi ya Arctic. Wataalamu hao wametahadharisha kwamba huenda idadi ya vifo ikaongezeka kutokana na joto kali katika siku zijazo.
Vyanzo:/DPA/AFP