1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu milioni 12 duniani kote ni wakimbizi wa ndani

Sylvia Mwehozi
16 Mei 2018

Ripoti iliyotolewa na wachunguzi wa kimataifa inaonesha kuwa migogoro iliwalazimisha watu karibu milioni 12 duniani kote kuwa wakimbizi ndani ya nchi zao mnamo mwaka jana ikiwa ni kiwango cha juu ndani ya miaka 10.

https://p.dw.com/p/2xnds
Syrien Flüchtlinge in Idlib
Picha: Reuters/O. Orsal

Jumla ya watu milioni 11.8 waligeuka wakimbizi wa ndani ya nchi zao wenyewe mwaka 2017, ikiwa ni karibu mara mbili ya watu milioni 6.9 waliopatwa na madhila kama hayo mwaka mmoja uliopita, kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha ufuatiliaji watu wakimbizi wa ndani cha IDMC na baraza la wakimbizi la Norway NRC.

"Hii ni idadi kubwa zaidi ambayo tumeweza kuirekodi katika miaka 10", alisema Mkuu wa IDMC Alekandra Bilak alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geneva.

Idadi hiyo mpya ya wakimbizi wa ndani inafanya jumla ya watu waliokimbilia katika maeneo mengine ndani ya nchi zao kutokana na migogoro kufikia milioni 40 duniani kote, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa.

Ruanda Kiziba Flüchtlingslager
Wakimbizi kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Picha: Reuters/J. Bizimana

"Idadi ya kushangaza ya watu wanaokimbia makazi yao kwa sababu ya mizozo na machafuko inapaswa kutufumbua macho sisi wote", amesema mkuu wa NRC Jan Egeland katika taarifa yake.

Ripoti hiyo imebaini kwamba asilimia 76 ya wakimbizi wa ndani mwaka jana imetokana na mizozo katika nchi takribani 10, ambapo Syria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Iraq pekee zina karibu nusu ya idadi hiyo.

Syria kwa mfano imeshudhudia watu milioni 2.9 wakiyahama makazi yao, wengi wao kwa mara ya pili au ya tatu na kufanya idadi ya watu waliokwama ndani katika taifa hilo lililokumbwa na vita kufikia karibu milioni 6.8.

Yemen, ambayo awali ilikuwa kinara katika orodha hiyo, haipo tena katika nchi 10 lakini Bilak amesisitiza kwamba hilo linatokana na ukosefu wa taarifa na kwamba hali katika nchi hiyo bado ni mbaya.

Bilak ameonya kwamba jumla ya wakimbizi wa ndani ya nchi zao duniani kote inaweza kuongezeka kuliko ilivyobainishwa na utafiti wao, akigusia kwamba kunakosekana taarifa za wapi walipo watu milioni 8.5 ambao waliripotiwa kurejea nyumbani au kupewa makazi mapya.

Tornado in den USA Dezember 2012
Athari za kimbunga nchini Marekani Picha: AP

Ripoti hiyo pia inasema watu milioni 18.1 katika jumla ya nchi 135 walipoteza makazi mwaka jana kutokana na majanga ya asili kama vile mafuriko, na vimbunga. Ukijumlisha na wale walioyapa kisogo makazi yao kwa sababu za migogoro, karibu watu milioni 31 hawakuwa na makazi mwaka jana ndani ya nchi zao wenyewe, ikiwa ni sawa na watu elfu 80 kwa siku.

Katika migogoro iliyotokana na majanga ya asili, nchi zilizoathirika zaidi ni China, Ufilipino, Cuba na Marekani. Vimbunga vitatu vikubwa katika ukanda wa Atlantiki mwaka jana, Harvey, Irma na Maria, hivyo pekee vilisababisha watu milioni 3 kukosa makazi. Wakati nchi zikihifadhi takwimu za watu waliokosa makazi kutokana na migogoro, taarifa za muda mrefu za watu waliokumbwa na majanga ya asili kwa ujumla hazipo.

Nchini Puerto Rico kwa mfano taarifa zinaonyesha kwamba watu 86,000 walikosa makazi kutokana na kimbunga Maria mwaka jana lakini hakuna taarifa wangapi hadi sasa hawana makazi.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/afp

Mhariri: Daniel Gakuba