1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu saba wauawa kwa shambulizi la Urusi nchini Ukraine

1 Oktoba 2024

Watu saba wameuawa nchini Ukraine katika shambulizi la Urusi lililolenga katikati ya mji wa Kherson ulio kusini mwa Ukraine. Hayo yamesemwa na ofisi ya mwendesha mashataka mjini humo mapema hii leo.

https://p.dw.com/p/4lHdD
Ukraine, Kyiv
Picha ya mlipuko wa droni ya Urusi katika mji wa Kyiv nchini UkrainePicha: Gleb Garanich/REUTERS

Watu saba wameuawa nchini Ukraine katika shambulizi la Urusi lililolenga katikati ya mji wa Kherson ulio kusini mwa Ukraine. Hayo yamesemwa na ofisi ya mwendesha mashataka mjini humo mapema hii leo.

Video iliyochapishwa na gavana wa mji wa Kherson uliopo kusini mwa Ukraine ilionyesha uharibifu mkubwa uliotokana na shambulizi la Urusi ambapo kwenye video hiyo vifusi na vioo vilivyovunjika vilionekana vikiwa vimetapakaa sokoni huku miili kadhaa ya watu ikiwa kwenye lami.

Soma zaidi.Ukraine yavunjwa moyo na Uswisi kuhusu mpango wa amani wa China na Brazil 

Mapema leo Oktoba mosi, Ofisi ya mwendesha mashtaka wa mji wa Kherson kupitia mtandao wa Telegram ilisema kuwa vikosi vya Urusi vilishambulia katikati mwa mji huo wa Kherson kwa mashambulizi ya  makombora.

Nikinukuu ujumbe wa telegram wa ofisi hiyo ulisema "Mashambulizi ya makombora yalifanyika karibu na soko la ndani na kituo cha usafiri wa umma. Hadi sasa, inafahamika kuwa watu saba, wanawake watatu na wanaume wanne wameuawa" mwisho wa kunukuu.

Hapo awali vikosi vya Urusi viliondoka katika mji huo mnamo Novemba 2022, na kurejea upande wa pili wa Dnipro, lakini bado vimeendelea kufanya mashambulizi makali katika mji huo wa kusini mwa Ukraine wa Kherson.

Mark Rutte aahidi kuisaidia zaidi Ukraine

Kwa upande mwingine vikosi vya Ukraine navyo vimeendelea kuudhibiti mkoa wa Urusi wa Kursk ingawa kwa sasa serikali ya Ukraine inasubiri kusikia kutoka kwa washirika wake wa magharibi ili kupatiwa msaada zaidi wa vifaa vya kijeshi.

 Brüssel | Mark Rutte
Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Mark Rutte akiwa na mtangulizi wake Jens Stoltenberg.Picha: Harry Nakos/AP/picture alliance

Wakati mapambano hayo yakiendelea kuchukua mkondo mpya, Mkuu mpya wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Mark Rutte amesema mapema leo kuwa anadhamiria kuandaa mpango wa siku zijazo utakaohakikisha kwamba Ukraine inapata msaada ili kukabiliana na vita vyake na Urusi.

Soma zaidi. Urusi yaishambulia tena Kiev kwa droni

Hapo jana kwenye mkutano wa Jumuiya hiyo ya Kujihami mjini Brussels,  Jens Stoltenberg ambaye amemaliza muda wake na kumpisha Mark Rutte alisema..

"Kila wakati tumeongeza msaada wetu na aina mpya za silaha, vifaru vya kijeshi, silaha za masafa marefu au ndege za kivita aina ya F-16, Warusi wanajaribu kutuzuia. Hawajafanikiwa. Kwa hivyo mashambulizi ya hivi karibuni yasituzuie sisi washirika wa NATO kuiunga mkono Ukraine.

Duru zinaarifu kuwa kwa sasa jeshi la Urusi limeongeza mashambulizi pia katika eneo la mashariki mwa Ukraine la Donetsk ambako linataka kuchukua udhibiti kamili kabla ya kuanza kwa msimu wa baridi.