Watu tisa washtakiwa Rwanda kwa kueneza habari za uongo
19 Oktoba 2024Washukiwa hao walifikishwa katika mahakama kuu ya Kigali huko Nyamirambo hapo jana, ambako walisomewa mashitaka ya kueneza propaganda kwa nia ya kusababisha mtazamo mkali wa kimataifa dhidi ya serikali ya Rwanda.
Pia walishutumiwa kwa kujiunga na shirika la uhalifu na njama ya kufanya uhalifu dhidi ya uongozi wa nchi hiyo.
Upande wa mashtaka waomba hukumu kali dhidi ya washtakiwa
Upande wa mashtaka uliiomba mahakama iwahukumu kifungo cha miaka 15 jela kwa washtakiwa saba na miaka 10 kwa wengine wawili.
Hakimu aamuru kikao kuendelezwa kwa faragha
Vyanzo kutoka mahakamani hapo vilisema wakati kesi ilipokuwa ikiendelea, hakimu wa mahakama hiyo aliamuru kuendelezwa faraghani na kuwaagiza waandishi wa habari, jamaa na baadhi ya wafuasi wa upinzani kutoka nje.
Kwa muda mrefu, upinzani wa kisiasa na uhuru wa kujieleza nchiniRwanda umekandamizwa chini ya utawala wa miongo mitatu wa Rais Paul Kagame.